Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman akizungumza baada ya kukabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo ya udereva katika chuo cha VETA mkoa wa Tanga. |
Na: Burhani Yakub,Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Chuo cha mafunzo ya ufundi stadi VETA mkoa wa Tanga kimeombwa kuanzisha mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ya udereva wa maroli ili madereva waliopo jijini hapa waweze kupata sifa ya kuyavusha maroli mapya yanayoingia nchini kupitia bandari ya Tanga kwenda nchi jirani za Maziwa Makuu.
Kufuatia meli kubwa zinazobeba shehena ya magari yanayopelekwa nchi za Maziwa Makuu kuanza kutia nanga katika bandari ya Tanga,imejitokeza changamoto ya idadi kubwa ya madereva waliopo jijini hapa kukosa sifa ya kuendesha maroli na hivyo kulazimu kuagizwa madereva kutoka nchi hizo kuyavusha hadi mipakani.
Ombi hilo wamelitoa walipozungumza na Mwandishi wa habari hizi baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga,Rajabu Abdurahmani kukabidhi vyeti vya madereva 71 wa mabasi ya abiria waliohitimu mafunzo katika chuo cha VETA kilichopo Jijini hapa.
Wamesema baada ya maboresho ya bandari ya Tanga tayari meli zenye shehena ya magari zimeanza kutia nanga katika bandari hiyo lakini wamiliki wa magari hayo wanazimika kuagiza madereva kutoka nchini kwao au jijini Dar es salaam kuyaendesha hadi mipakani.
"Wengi leseni zetu ni ndogo haziruhusu kuendesha maroli makubwa,chuo cha VETA hapa Tanga hakina kozi za udereva wa maroli zaidi ya mabasi na magari mengine ya abiria ndiyo maana tunaomba VETA Tanga kianzishe kozi hizi kwa sababu ya uhitaji uliopo"amesema Bakari Mussa.
Mbunge wa Jimbo la Tanga,Ummy Mwaimu amesema hitajio la mafunzo ya udereva wa maroli ni kubwa kwa sababu meli kubwa kutoka nchi za Ulaya zitakuwa zikitia nanga katika bandari ya Tanga kila wiki kushusha shehena za maroli ni vyema hata madereva wa Tanga wanufaike na fursa hiyo.
"Wiki hii meli kutoka China imepitia Singapore na kuja bandari ya Tanga,imeshusha maroli mengi yanayopelekwa Zambia lakini madereva wanaoyapeleka wametoka Zambia wanasema wamewatafuta wa Tanga wengi leseni zao haziwaruhusu kuyaendesha...nitapigania ili mafunzo yaanze kutolewa chuo cha VETA hapa Tanga"amesema Ummy.
Mkuu wa mkoa wa Tanga,Balozi Dkt Batilda Buriani amesema changamoto hiyo ataifanyia kazi ili madereva wa Tanga nao waweze kuchangamkia fursa hiyo.
"Awali walikuja madereva hawa waliohitimu leo kunilalamikia kuwa wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara nilipofuatilia nikabaini kuwa tatizo ni kukosa mafunzo nikamuomba Mwenyekiti wangu wa CCM mkoa akakubali na akalipia ada za madereva 71...niahidi kuwa hata hili la madereva wa maroli nitalishughulikia"amesema Batilda Buriani.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Abdurahman amesema kuna kila sababu ya wakazi wa Tanga wakiwamo madereva kunufaika na uwepo wa bandari katika eneo lao na kuitaka VETA kuanzisha mafunzo katika chuo cha VETA Tanga.
"Nikiwa kiongozi katika mkoa wa Tanga sitakubali kuona wakazi wa Tanga wanakosa kunufaika na raslimali pamoja na fursa zilizopo hapa,nitashirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha tunafanyia kazi changamoto hii"amesema Rajabu
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi kuhusiana na ombi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha VETA mkoa wa Tanga,Gideon Olerlairumbe,Afisa raslimali watu,Josephine Mahonge amesema wamelipokea na watalifanyia kazi.
"Ni kweli VETA mkoa wa Tanga kozi tunazoendesha ni za madereva wa mabasi makubwa na madogo,tax kusafirisha watalii ambao wana leseni kuanzia class C Plain,C1,C2,,C3 na boda boda wenye leseni Class A lakini madereva wa maroli ambao leseni zao ni class E mafunzo yao yanatolewa katika vyuo vilivyopo Mikoa mingine... lakini niahidi kuwa kuanzisha hapa Tanga inawezekana,tutawasilisha makao Makuu ili kulifanyia kazi"amesema Josephine.
Amesema hitajio la kozi ya madereva wa maroli katika chuo cha VETA mkoa wa Tanga,litaleta ufumbuzi wa changamoto ya uhaba wa madereva kwa sababu wengi wao watapata kazi za kuyapeleka hadi kwenye mipaka ya nchi jirani ama kiyafikisha kwenye husika na hivyo kujipatia fedha za kukidhi mahitaji ya familia zao.
MWISHO
No comments:
Post a Comment