Wanavijiji Pangani wajengewa uwezo mchakato wa bajeti - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 26 October 2024

Wanavijiji Pangani wajengewa uwezo mchakato wa bajeti

Pichani ni Wakazi wa Kijiji cha Bweni Wilaya ya Pangani mkoa wa Tanga wakiwa katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua fursa na vikwazo vya maendeleo na mchakato wa bajeti katika kuboresha elimu yaliyoendeshwa na Shirika la Tree Of Hope kwa kushirikiana na mtandao wa elimu Tanzania) Tenmet).


Picha zote na Burhani Yakub







Burhani Yakub, Pangani.

maipacarusha20@gmail.com

Wakazi wa Vijiji na vitongoji vya Wilaya ya Pangani wamejipanga kushiriki mchakato wa kupanga bajeti za maendeleo yakiwamo ya sekta ya elimu ili changamoto zinazowakabili ziweze kujulikana na kutatuliwa.


Wamesema kitendo cha kutoshiriki mikutano ya vijiji na vitongoji kumechangia changamoto zao kutoibuliwa wakati wa uwasilishaji wa bajeti kwenye ngazi za Wilaya mkoa na Taifa.


Walitoa ahadi hiyo baada ya kushiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua fursa na vikwazo vya maendeleo na mchakato wa bajeti katika kuboresha elimu kwa wakazi wa Vijiji na vitongoji vya Pangani Magharibi, Miembeni, Mwera, Bweni na Boza yaliyotolewa na Shirika la Tree Of Hope kwa kushirikiana na Mtandao wa elimu Tanzania (Tenmet).


Hadija Mkufya ambaye ni mkulima na mjasiiliamali wa Kijiji cha Mwera amesema wengi wao walikuwa wakikwepa kushiriki mikutano ya kila miezi mitatu na mikutano mikuu kwa kudhani haiwahusu lakini baada ya kupata mafunzo wamebaini hata bajeti inayojadiliwa na kupitishwa bungeni inatokana na kuibuliwa kwenye vitongoji.


"Hatukuwa tukijua kwamba bila ya sisi kuibua changamoto za miundombinu, hawatajua kama barabara za mashambani ni mbovu, kuna uhaba wa walimu, tunahitaji shule ili wanafunzi wasibakwe kwa kutembea umbali mrefu...lakini sasa tumehamasika tutashiriki mikutano na ispoitishwa tutahoji"amesema Abdurahaman Mwinyijia wa kitongoji cha kikokwe Kijiji cha Bweni.


Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwera, Mariam Mkwato amesema mafunzo yamesaidia kuwajengea uelewa wakazi wa eneo lake kuhudhuria mikutano ili waweze kuibua fursa na vikwazo vinavyowakabili ili kurahisisha uandaaji wa bajeti za kila sekta.


"Wengi hawahudhurii mikutano lakini ndiyo wakwanza kulalamika...mafunzo haya yametusaidia hata sisi watendaji"amesema Mariam.


Mratibu wa miradi wa Shirika la Tree Of Hope, Good luck Malilo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wakazi wa Vijiji vya Wilaya ya Pangani wa kutambua fursa na vikwazo vya maendeleo na mchakato wa bajeti katika kuboresha. elimu.


Lengo la pili ni kuwajengea uwezo wa kuzipa kipaumbele,hatua zote za mchakato wa bajeti ili miradi inayopelekwa bungeni iwe inatoka kwenye ngazi za chini.


"Mafunzo haya ambayo tumeanza na vijiji vya Pangani Magharibi, Miembeni, Mwera,Bweni,na Boza tunaendesha Tree Of Hope kwa kushirikiana na Mtandao wa elimu Tanzania (Tenmet).


Katika mafunzo hayo wa washiriki walifundishwa mchakato wa bajeti unavyoanzia katika ngazi za ngazi za halmashauri za vijiji,mikutano mikuu ya vijiji,kamati za maendeleo za kata, Halmashauri ya Wilaya,mikutano kamati za ushauri za maendeleo za Wilaya ( DCC) mkoa ,(RCC),Serikali kuu hadi Bungeni inakopitishwa kwa ajili ya utekelezaji.


MWISHO



No comments: