CCM YATAMBA KUSHINDA SIMANJIRO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 16 November 2024

CCM YATAMBA KUSHINDA SIMANJIRO

 



Na Mwandishi wetu, Simanjiro


KATIBU wa CCM mkoa wa Manyara, Idd Mkowa amesema chama hicho kinatarajia kushinda kwa kishindo uchaguzi wa serikali za mitaa Wilayani Simanjiro kwani wanajivunia utekelezaji wa ilani ya chama hicho kupitia miradi ya maendeleo.


Kwenye Wilaya ya Simanjiro CCM itapambana na Chadema katika vitongoji 28 na vijiji sita


Mkowa ameyasema hayo mji mdogo wa Orkesumet wiilayani Simanjiro, akizungumza mbele ya Katibu wa NEC- Orgainezesheni wa CCM Taifa ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM kwenye uchaguzi Issa Haji Gave, katika kikao cha tathmini ya wagombea wa CCM waliopitishwa kugombea nafasi mbalimbali za serikali za mitaa.


"Tuna imani kubwa na jamii ya Simanjiro kuichagua CCM, kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika ikiwemo ya sekta ya afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu ya barabara," amesema.


Amesema kwenye wilaya ya Simanjiro yenye vijiji 56 CCM imepita bila kupingwa vijiji 50 na chama kimoja cha upinzani Chadema wameweka wagombea kwenye vijiji sita.


Amevitaja vijiji vilivyopata upinzani ni Landoto kata ya Msitu wa Tembo, Naepo kata ya Naisinyai, Namalulu kata ya Naberera, Ngorika na Nyumba ya Mungu kata ya Ngorika na Ngage kata ya Loiborsoit.


Amesema kwa upande wa vitongoji 277 vya wilaya ya Simanjiro, CCM imepita bila kupingwa vitongoji 249 na vitongoji 28  vimepingwa na wagombea wa Chadema.


“Kwenye kata ya Mirerani vitongoji vyote 12 vimewekewa wagombea wa Chadema, kata ya Endiamtu vitongoji 11, kata ya Orkesumet vitongoji viwili, Msitu wa Tembo vitongoji viwili na kata ya Ngorika kitongoji kimoja,” amesema.


Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer amesema hana wasiwasi na chama hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwani anatarajia watapata ushindi wa kishindo.


"Wenye macho wameona na walio na masikio wamesikia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Kiria.


Amesema mara baada ya tarahe ya kuanza kampeni itakapofika CCM itafanya kampeni kwenye hayo ili kuelezea maendeleo yaliyofanyika.


Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amesema ataweka kambi kwenye maeneo yaliyo na wagombea wa upinzani ili kuhakikisha CCM inashinda.


"Kwenye kata za Mirerani, Endiamtu na maeneo mengine yenye upinzani msiwe na shaka kwani CCM itashinda kwa kishindo kutokana na kazi kubwa iliyofanyika kupitia miradi ya maendeleo," amesema Ole Sendeka.


MWISHO

No comments: