DC KAGANDA AWATAKA MADIWANI KUHAMASISHA UKUSANYAJI WA MAPATO, KUCHOCHEA MAWNDELEO YA BABATI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 2 November 2024

DC KAGANDA AWATAKA MADIWANI KUHAMASISHA UKUSANYAJI WA MAPATO, KUCHOCHEA MAWNDELEO YA BABATI

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda,  akizungumza na madiwani wa halmashauri ya Babati





 Na: Epifania Magingo, Manyara 


maipacarusha20@gmail.com 


Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, ameshiriki kikao cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mji ambapo  Kwenye  hotuba yake kwa madiwani, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ili kuchochea maendeleo ya Wilaya.


Kaganda amewahimiza madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusaidia upatikanaji wa mapato kwa kila eneo wanaloongoza jambo ambalo litasaidia kuongeza mapato ya ndani na ni hatua muhimu katika kuboresha miradi ya kijamii na miundombinu ndani ya Wilaya.


“Tutakusanya fedha nyingi na mtaweza kufanya kazi kubwa sana ndani ya Halmashauri, mkiweza kukusanya zaidi mtaweza kufanya kazi kubwa zaidi hata ninyi mtaendelea kufurahia na mtaweka alama nzuri". amesem


Katika suala la kilimo, Kiongozi huyo ametoa rai kwa Madiwani kutoa ushirikiano katika kuanzisha vyama vya ushirika vya "Amkosi" ambavyo vitawawezesha wakulima kupata ruzuku na fursa za kuuza mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la  kuwainua wakulima kiuchumi na kuhakikisha wanapata bei nzuri za mazao yao.


Aidha, Kaganda pia ameeleza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kukemea vikali tabia ya ukataji miti kiholela bila kibali kutoka Serikalini na kuwasihi  Madiwani kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria za utunzaji mazingira ili kuboresha ubora wa mazingira ya Babati kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Akizungumzia umuhimu wa kuweka kipaumbele kwenye utoaji wa chakula mashuleni kwa wanafunzi, Kaganda  ametoa angalizo juu ya uhifadhi salama wa vyakula ili kuepuka athari za sumu kuvu huku akiwaomba Madiwani kuwafahamisha wazazi na walezi kuhusu suala hilo ili kuimarisha usalama wa afya ya wanafunzi.


Kiongozi huyo pia ametumia fursha hiyo, Madiwani kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mtaa 27 November na kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi huo ili kuimarisha demokrasia ya eneo la Babati.


Mkuu wa Wilaya Kaganda,ametoa wito kwa Madiwani hao kuwa na mshikamano na ushirikiano baina yao  na Halmashauri ili kufanikisha utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Babati.

No comments: