Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite kwa namna inavyosaidia jamii kupitia miradi ya maendeleo (CSR).
Makota akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani amesema kampuni ya Franone inatoa misaada mbalimbali kwa jamii ila inaishirikisha serikali.
Amesema hivi karibuni kampuni hiyo imechangia shilingi milioni 20 kwenye zahanati ya kijiji cha Naepo na shilingi milioni 60 kwa ajili ya miradi ya elimu mji mdogo wa Mirerani na kata ya Naisinyai.
"Unapotoa misaada kwa jamii (CSR) ishirikishe Serikali na tutatoa na cheti na siyo kusaidia mtu mmoja kwani jamii haitanufaika ni kama umeenda kwenye dansi ukatajwa jina papaa fulani ukagawa fedha kwa waimbaji," amesema Makota.
Hata hivyo, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, imepanga kutekeleza miradi 18 ya thamani ya Sh1.354 bilioni kupitia fedha za wadau wa madini ya Tanzanite kuwajibika kwa jamii (CSR).
Makota amesema miradi hiyo 18 itajengwa kwenye kata tofauti kwa lengo la jamii ya Simanjiro kunufaika kupitia rasilimali inayowazunguka ya madini ya Tanzanite.
Ameitaja miradi hiyo ni ujenzi wa zahanati ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ya thamani ya Sh150 milioni, ujenzi wa bweni la shule ya msingi Saniniu Laizer Sh90 milioni na ukarabati madarasa manne shule ya msingi Songambele Sh40 milioni.
Ameitaja miradi mingine ni ujenzi wa kituo cha afya Ngorika Sh250 milioni, uendelezaji wa kituo cha afya Komolo Sh230 milioni, uendelezaji kituo cha afya Mirerani Sh27 milioni na uendelezaji nyumba ya mwalimu shule ya msingi Engonongoi Sh70 milioni
"Miradi mingine ni ukamilishaji nyumba ya walimu shule ya msingi Einot Sh30 milioni na ujenzi wa bweni la wavulana shule ya msingi Ruvu Remit Sh100 milioni na uboreshaji machinjio mji mdogo wa Mirerani," amesema Makota.
Amesema miradi mingine ni ujenzi wa bweni la wavulana shule ya sekondari Eng'eno Sh80 milioni, ujenzi wa nyumba ya mwalimu shule ya sekondari Embris Sh26 milioni na ukamilishaji madarasa manne shule ya msingi Langai Sh40 milioni.
Ameitaja miradi mingine ni ukarabati madarasa manne shule ya msingi Loiborsiret Sh40 milioni, kukamilisha nyumba ya mwalimu shule ya msingi Mbuko Sh56 milioni, kumaliza nyumba ya watumishi kituo cha afya Nadonjukin Sh35 milioni na uendelezaji kituo cha afya Terrat Sh70 milioni.
Ofisa madini mkazi (RMO) Mirerani, Nchagwa Chacha Marwa, amesema uchangiaji maendeleo kwa jamii CSR ni takwa la kisheria hivyo wachimbaji madini watekeleze hilo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amewashukuru wadau wa madini waliohudhuria kikao hicho kwani watapokea maoni yao katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite Eliaman Mgala amesema elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwao ili waelewe namna ya kuchangia miradi ya maendeleo kwa jamii ya wilaya hiyo.
"Hata kwenye nyumba za ibada kuna sadaka zinatolewa hivyo wachimbaji tunapaswa kuelezewa zaidi ili tuweze kushiriki kuchangia miradi ya maendeleo katika wilaya hii ya Simanjiro," amesema Mgala.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani Peter Loiting'id Laizer amesema baadhi ya wachimbaji huwa wanachangia maendeleo ila hawatambuliki kiserikali.
"Wachimbajia wengine huwa wanaombwa misaada mbalimbali ya maendeleo na jamii inayowazunguka ila hawatambuliki kwa sababu hawatoi taarifa serikalini," amesema Laizer.
MWISHO
No comments:
Post a Comment