EWURA YATAKIWA KUFANYA UCHAMBUZI WA KINA KUKABILIANA NA UPOTEVU WA MAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 11 November 2024

EWURA YATAKIWA KUFANYA UCHAMBUZI WA KINA KUKABILIANA NA UPOTEVU WA MAJI

 






Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetakiwa kufanya uchambuzi wa kina kukabiliana na changamoto ya  upotevu na upatikanaji wa maji nchini pamoja na kuongeza mbinu katika maeneo ya utafiti ya matumizi ya nishati safi na usafi wa mazingira.


Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Nishati Dk James Mataragio   akizungumza hayo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Dotto Biteko,katika kikao Cha tatu cha Baraza la wafanyakazi wa EWURA kinachoendelea mjini Morogoro .


Alisema pamoja na kwamba Wizara inambua mchango wa  Ewura katika kuhakikisha viwango vya ubora wa maji vinapatikana ili kumpa mwananchi huduma stahiliki bado kuna jukumu kufanya hasa kwa upotevu wa maji na namna ya kuhakikisha maji yanapatikana.


"EWURA inapaswa kuendelea kusonga mbele, muwe na mikakati ya kuimarisha ujuzi,maarifa ya kuongeza mbinu hususani kwa maeneo ya utafiti,matumizi bora ya Nishati,Nishati jadidifu na Hali ya sasa ya soko la mafuta,gesi asilia na usalama wa usafi wa mazingira,"alisema.


Aidha alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha ifikapo 2034 watanzania asimia 80 watumie Nishati safi ya kupikia.


Alisema maeneo ya vijijini bado yana uhitaji wa vituo vya mafuta na hamasa ya matumizi ya Nishati safi  ya kupikia ujenzi wa vituo kupewa kipaumbele ambayo ni agenda ya kipatifa ya Nishati safi ya kupikia.


Baada ya ufunguzi wa kikao Cha baraza hilo la wafanyakazi wa Ewura, kukifanyika uzinduzi wa Mradi wa Nishati Safi na Salama ya kupikia katika shule ya sekondari ya Morogoro(MoroSec) na kambi ya kuelekea wazee ya Fungafunga Morogoro.


Mkurugenzi mkuu wa EWURA Dk James Andilile alieleza kuwa Ewura imekuwa ikifanya urejeshaji kwa jamii kila mwaka ambapo kwa shule ya sekondari Morogoro wamefunga majiko sita na mitungi mitatu ya gesi ya kupikia huku katika Kambi ya wazee Fungafunga wamefunga majiko matatunna mitungi mitano ya gesi yenye thamani ya sh 40 milioni.


Andilile alisema kufungwa kwa majiko na mitungi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na kuwa na manufaa makubwa na kwamba matumizi ya gesi yanapunguza muda wa kupikia.


"Ujenzi wa miundombinu hii itakuwa chachu kwa shule nyingine na Serikali unafanya jitihada ya kuhakikisha matumizi ya Nishati safi na salama inaenea nchi mzima na kuweka malengo yaliyowekwa yanatimia kwa asilimia kubwa,"alisema.


Mkuu wa sekondari ya Morogoro Boniphace Gonja akishukuru kufungwa kwa miundombinu hiyo alisema awali walikuwa wakitumia kiasi cha shillingi 2.6 milioni kwa mwezi kwa ajili ya kuni na magogo ya kupikia chakula cha wanafunzi.


Gonja alisema kwa uwekezaji huo watapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ambapo wanatarajia kutumia kiasi cha shillingi 1.6 ambapo sh 1 milioni itasaidia kwenye matumizi mengineyo.


Aliahidi kulinda na kutunza mazingira na kuendelea kutumia Nishati safi na salama ya kupikia.




No comments: