Na: Mwandishi wetu, Meatu
maipacarusha20@gmail.com
Taasisi ya uhifadhi ya Fredkin Conservation Fund (FCF) kupitia kampuni yake ya Mwiba Holdings Ltd, iliyowekeza shughuli za utalii na Uhifadhi wilayani Meatu mkoani Simiyu, imetoa kiasi cha dola 46,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi million 120 kufadhili masomo ya wanafunzi mwaka 2023 na mwaka 2024.
Wanafunzi wanafadhiliwa masomo kuanzia sekondari hadi vyuo vikuu wengi ni kutoka Kaya Masikini za wilaya ya Meatu.
Meneja wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii wa FCF wilayani Meatu, Sylvester Bwasama alitoa taarifa hiyo jana wakati wa mafunzo ya Stadi za Maisha kwa wanafunzi wa sekondari wilaya ya Meatu.
Bwasama alisema FCF kuanzia mwaka Jana 2023 ilitoa kiasi ya dola 23,000 kufadhili masomo na mwaka huu 2024 imetoa dola 23,000.
"Wanafunzi ambao tunawafadhili wengi wanatoka Kaya Masikini lakini wamefaulu vizuri masomo yao na tunafadhili hadi vyuo vikuu"alisema
Alisema lengo la FCF kutoa ufadhili ni kuwawezesha wanafunzi wengi kusoma na kuwa na elimu bora na baadae kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi wa mazingira na wanyamapori hapa nchini.
Akizungumzia mafunzo ya Stadi za Maisha alisema Wanafunzi zaidi ya 1000 katika shule za sekondari wilaya ya Meatu ,wameanza kupata mafunzo.
"Wanafundishwa masuala ya kupinga ndoa za utotoni, masuala ya uzazi, uhifadhi na ujasiriamali"alisema
Alisema bado katika wilaya hiyo kuna changamoto ya wanafunzi kupewa ujauzito wakiwa shuleni, utoro na baadhi kukatisha masomo na kwenda kuchunga mifugo.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo, Abubakar Mutoka na Pascal Steven, wakitoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mbugayabanghya na Meatu Sekondari, waliwataka wanafunzi kuwa malengo katika masomo yao.
Mutoka alisema, Wanafunzi wanafursa ya kuandaa vizuri maisha yao ya baadae kuanzia shuleni pale ambapo watasoma kwa makini na kuwa na malengo ya muda mfupi wa kati na ya muda mrefu.
"Shuleni ndipo mnaanza kuandaa maisha yenu ya baadae, someni achaneni na vitendo ambavyo vitaharibu ndoto zenu" alisema
Steven aliwataka wanafunzi wa kike kujitenga na ushawishi wa vitendo vya ngono kwani vitaharibu malengo Yao.
"Kuna changamoto ya vijana hasa wa bodaboda kuwasumbua achaneni nao, kuweni wakali kwani wataharibu maisha yenu"alisema
Kwa upande wake Afisa mazingira wa FCF, Lameck Stanslaus aliwataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri wa mazingira na kupinga masuala ya ujangili.
"Meatu Leo tuna shule za kutosha, tuna madarasa mazuri na mazingira mazuri ya kusoma kutokana na Uhifadhi hivyo wanafunzi muwe mabalozi wazuri wa kutunza mazingira"alisema
Mafunzo ya stadi za Maisha yanaendelea katika wilaya hiyo na lengo la kubadili mitazamo hasi kwa wanafunzi hasa katika masuala ya maisha Yao lakini pia kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.
Wilaya ya Meatu inapakana na hifadhi ya Ngorongoro na hifadhi ya Taifa ya Serengeti pia kuna mapori kadhaa ya akiba na jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori ya makao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment