CORDS Kuunda Mtandao wa wanawake jamii za Asili kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi Nchini - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 22 November 2024

CORDS Kuunda Mtandao wa wanawake jamii za Asili kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi Nchini

 






Nan'gida Laizer Toka Wilayani Longido akielezea umuhimu wa mtandao huo kwa wanawake Jamii za Asili

Na Mwandishi Wetu, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Wanawake Jamii za Asili Nchini Tanzania wameelezea kukabiliwa na changamoto za upungufu wa chakula na malisho ya mifugo kutokana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.


Wanawake hao kutoka jamii za wahadzabe, Wamasai, wabarbaigi, wadatoga na waakei wanasema Upungufu huo umesababishwa na ukame katika maeneo mengi ya jamii hizo na hivyo kuathiri maisha ya wanawake wa jamii za Asili.


Akifungua Kongamano la siku mbili la wanawake wa jamii za Asili, Mkurugenzi wa shirika la utafiti na maendeleo ya jamii (CORDS) Lilian Looloitai amesema kuwa wanawake wa jamii za Asili wanakabiliwa na athari za mabadiliko ya Tabianchi yaliyopelekea kuwepo na vikwazo vya kiuchumi na kijamii.


Amesema mabadiliko ya Tabianchi yameathiri maisha ya kila Siku kwa wanawake wafugaji na waokota matunda na hivyo ni muhimu kwa wanawake hao kuwa na mtandao wa pamoja utakaosaidia kufikia malengo ya uongozi na maendeleo ya uchumi kwa jamii hizo.


Mtandao huo utatoa fursa kwa wanawake wa Asili kuwa na ujasiri wa kugombea nafasi za uongozi pamoja na kuweka mikakati wa Mawasiliano ya jamii zote za Asili Nchini.

 Mjumbe wa Bodi ya CORDs Adam ole Mwarabu akizungumza katika kongamano hilo alitaka wanawake wa jamii ya asili kuendelea kutunza mila na tamaduni zao.     

Ole Mwarabu amesema licha ya maendeleo makubwa ya Sayansi na teknolojia bado kuna haja ya kuendelezwa mila na desturi za jamii za asili.

 Amesema jamii za asili zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwepo masuala ya mabadiliko ya tabianchi lakini umoja na mshikamano utasaidia kutatua changamoto hizo.  

Regina Majawa Gapchojiga kutoka jamii za wa barbaigi anasema kuwa wanawake wa jamii hiyo Wameathiriwa mno na mabadiliko ya Tabianchi yaliyosababisha mifugo kufa na hivyo kulazimika kuhamisha iliyopo kwenda kutafuta malisho nje ya wailaya ya Hanang' na hivyo kuathiri uchumi wa kaya zao.

Nan'gida Laizer Toka Wilayani Longido amesema changamato za jamii za asili ni nyingi hivyo CORDS kuwakutanisha ni jambo jema sana. Nan'gida alisema miongoni mwa changamoto ambazo wanakabiliana nazo ni athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Naye  Janeth Kamunyu  Toka shirika la Kinyok Indigenous Pastoralists women Organization (KIPWO) lililopo Mvomero Mkoani Morogoro anasema Kongamano hilo litawasaidia kuwa na sauti ya pamoja kujua changamoto zinazowakabili wanawake wa Asili Nchini Tanzania. 


Afisa Masuala ya jinsia wa shirika la CORDS Martha Katau  amesema kongamano hilo ni muhimu kwani limekutanisha wanawake wa jamii za asili nchini.  Katau amesema wanajadiliana utatuzi wa changamoto za jamii za asili  nchini.


Anna Matinda Afisa Utawala CORDS amesema wanaimani kongamano hilo litasaidia kuwaunganisha wanawake na kuwa na sauti moja katika utetezi wa jamii za asili.    Alisema CORDS imeandaa kongamano hilo la kwanza pia kuwatambua wanawake wa jamii za asili shughuli zao mbalimbali na jinsi ya kuwaunganisha.


Kongamano hilo ni la kwanza kwa wanawake wa jamii za asili ambalo linatarajiwa kufanikisha kuanzishwa kwa mtandao wa wanawake wa jamii za asili nchini Tanzania.

 

No comments: