Na Epifania Magingo, Manyara
maipacarusha20@gmail.com
Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wa maendeleo hapa Nchini za kuendelea kupinga vitendo vya kikatili vinavyofanyikia dhidi ya wanawake na watoto imeelezwa kuwa jamii yenyewe imekuwa na kutokua na muamko wa kutoa ushirikiano kwa Mamlaka husika ikiwemo Jeshi la polisi ili kutokomeza vitendo hivyo.
Baadhi wa wadau wa kupambana na kupinga vitendo hivyo wameeleza hali halisi ya matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwenye hafla ya ufunguzi wa siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia iliyofanyika Wilaya Babati Mkoani Manyara ambapo wamesema Miongoni mwa wazazi wamekua wakiwanyasasa watoto wao kingono kinyume na Sheria na kutozingatia malezi Yao kwa ujumla.
" Athari ni kubwa katika jamii watoto wananyanyasika, tunajitajidi kutafuta haki, utakuta baba hajishughulishi na chochote ahudumii familia, wamama wanateseka, wababa hawajali majukumu Yao, Mkoa wetu unashika nafasi ya juu kwa matukio ya ukatili, naomba Serikali iongeze nguvu kutusaidia Kina mama wanateseka na watoto kwa vitendo hivyo". amesema Rehema Omary
" Kuna watoto wanakatiliwa wananyimwa Elimu mfano jamii ya kimasai, matukio ni mengi, kwa hiyo naamini siku hizi 16 zitamsaidia mama na mtoto wa kike kupata uelewa wa kujikwamua kutoka kwenye ukatili wa kijinsia ". amesema victoria sumae
Mwakilishi kutoka Kitengo Cha Dawati la Jinsia Wilaya ya Babati Mkoani Manyara Inspeka Daud Danyesi amesema licha ya kuhakikisha kesi zote zinazoripotiwa za vitendo vya ukatili wa kijinsia zinafanyiwa upelelezi na kuchukuliwa hatua lakini pia amesema wanakabiliwa na changamoto ya Jamii kutotoa ushirikiano kikamilifu wa kutoa ushahidi ili kesi hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi.
"Mashahidi muhimu katika kesi hizi za ukatili huwa hawafiki kwaajili ya kutoa ushahidi, wakati mwingine wamekua wakikimbia kabisa, nyingine wamekua wakimalizana nyumbani, mtuhumiwa anakamatwa lakini ndugu au mhanga wa tukio lile wanaitana na wazee wanamalizana nyumbani, sasa kesi inakua inashindwa kupata mafanikio".amesema Danyesi
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoà wa Manyara Anna Fisso amesema asilimia 60 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokea katika mazingira ya nyumbani kwakua wanaofanya vitendo hivyo ni ndugu wa karibu ambao wanaaminiwa na familia huku akieleza kuwa Jamii imekua ikizingatia mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati ikiwemo suala la ukeketaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya ameiomba Serikali ya Mkoa wa Manyara kuwashirikisha Waandishi wa Habari kikamilifu katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Katika hafla ya ufunguzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto Askofu Petter Konki wa Kanisa la Elimu Pentecoste ambaye alikua Mgeni Rasmi amesema wananchi wanapaswa kuungana na Serikali kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa sahihi mahakamani wanapobaini vitendo vya kikatili katika Jamii inayowazunguka.
"Kutokomeza ukatili wa kijinsia ni jitihada za kuleta maendeleo, hatuezi kufanikisha maendeleo kama hatuwezi kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia, mafanikio ya maendeleo ni kutokomeza ukatili pia".amesema Konki.
Amesema, pamoja na jitihada za kupambana na vitendo vya ukatili katika Jamii pia tunapaswa kubadili mifumo ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia ikiwemo kulinda mifumo ya wahanga wa vitendo vya ukatili na kulinda taarifa za wahanga pia kutoa misaada ya kisheria na kisaikolojia kwa wahanga hao.
Takwimu za matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa Mkoa wa Manyara imetajwa kuwa kwa mwaka 2022 wahanga wa ukatili 5912, Januari 2023 Hadi Disemba matukio ,8360 na 2024 Januari Hadi Octoba matukio7893.
Kampeni ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Manyara kwa mwaka huu imebebwa na Kauli mbinu inasemayo "kufikia miaka 30 tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana".
No comments:
Post a Comment