Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema uongozi wowote lazima ufuate misingi mitatu Ushirikishwaji, Uamuzi unaozingatia Ushahidi pamoja na kuzingatia mslahi ya Taifa.
Ameeleza hayo baada ya kutunikiwa Shahada ya Uzamili ya heshima katika uongozi (Udaktari wa Heshima) na mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk Ally Mohamed Shein ambapo Shahada hiyo ni ya kwanza kutolewa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho.
Aidha Rais Samia alisisitiza kuwa viongozi katika ngazi yoyote lazima utoke Moyoni na uwe wenye maadili pamoja na baraka kutoka kwa Mungu.
Rais Samia Suluhu akisimulia alivyosoma katika Chuo Kikuu hicho alieleza kuwa enzi zao wakati mwingine walikuwa wakitumia Koroboi kwani umeme ulikuwa ukikatika mara kwa mara.
"Nilipofika tu Mzumbe nilikaa kwenye bweni Moja la Matola mpaka namaliza, kwa sisi tunatoka pwani tulikuwa na wakati mgumu sana umeme unapokatika unaona macho ya fisi tu kwenye Msitu mnene, lakini tulisoma na tumefika hapa tulipo,"alisema Rais Samia Suluhu.
Pia aliwataka wanafunzi wa Sasa kusoma kwa bidii kutokana na kuwepo kwa mazingira Bora ya elimu kwa sasa na kwamba hakuna sababu ya wanafunzi hao kutosoma vizuri.
Mkuu huyo wa nchi alisema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi kwenye Teknolojia na tafiti zenye manufaa ili kuimarisha elimu ya juu na kuwawezesha wahitimu kushindana kwenye nyanda mbalimbali kikanda na kimataifa.
"Tutaendelea kutafuta Fedha kuwekeza kwenye elimu ili kujibu changamoto za kikanda na kimataifa zilizopo," alisema Rais Samia Suluhu akizungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu Mzumbe baada ya kutunukiwa shahada ya udaktari wa heshima katika Uongozi.
Awali kabla ya kutunikiwa Udaktari huo wa Heshima kwa Rais Samia, ulitolewa wasifu na uzoefu wake na kusomwa na Profesa Cyriacus Binamungu ikiwemo kuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa Rais na mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania.
Shahada hiyo ya udaktari wa heshima ni ya tano kwa Rais Samia kutolewa tangu alipoingia madarakani ambapo shahada nyingine nne ametunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania), Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (India) na Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Uongozi wa chuo Kikuu cha Mzumbe kimefanya maamuzi sahihi ya kumtunukia shahada ya Udaktari wa heshima kwani anastahili kutokana na mambo makubwa.
Alisema Rais Samia mara baada ya kuapishwa mwaka 2021 alikuja na agenda ya mageuzi ya elimu na aliendelea kusimamia hilo na badae ajenda hiyo ikaletwa na Umoja wa Mataifa.
" hii inaonyesha Rais Samia amekuwa akitangulia
Mbele ya Mataifa mengine" alisema Waziri Mkenda
Akitoa nasaha kwa wahitimu Mlau wa Mahafali Profesa Hawa Tundui aliwataka wahitimu hao kuvua Majoho na kofia baada ya Mahafari na kwenda kufanya kazi yoyote iliokuwa halali bila kuchagua.
Aidha alisema nchi ya Tanzania ajira ni adimu lakini ina rasilimali nyingi na kwamba changamoto iliopo kwa vijana wengi wanaendelea kuvaa majoho jambo linalowafanya kushindwa kutumia vipaji vyao na hivyo kubaki na mtazamo wa na kushindwa kufanya kazi zingine wakisubiri kuajiriwa.
"Ndio maana wapo wanaokaa mtaani bila kufanya kazi, mimi nilihitimu shahada ya kwanza mwaka 1995, nikaenda kufuga kuku hadi mwaka 1997 nilipopata ajira hapa Mzumbe" alisema.
Katika mahafali hayo ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe jumla ya wahitimu 2,817 wamehitimu Shahada za Uzamivu(Doctor of Philosophy) wakiwa 12, Stashahada pamoja na Astashahada.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment