Mwandishi wetu,Loliondo.
maipacarusha20@gmail.com
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Kisheria Ngorongoro (NGOLAC) wamekabidhi magodoro na vifaa kadhaa kwa gereza la Loliondo wilaya ya Ngorongoro mkoa Arusha kwa ajili ya wafungwa.
Gereza la Loliondo ni moja ya gereza kongwe na lenye historia kubwa, lilijengwa na kuanzishwa mwaka 1922, ikiwa ni gereza la tatu nchini Tanzania (kabla pakijulikana kama Tanganyika kwa mwaka 1922).
Akizungumza na viongozi wa THRDC na NGOLAC, Mkuu wa gereza la Loliondo, SP George Osindi alisema kwa sasa, gereza hilo lina wafungwa 80, na mahabusu 21.
SP Osindi, ameelezea kuwa gereza hilo limejitosheza kwa asilimia 90 kwa upande wa maeneo ya kuhifadhi wafungwa.
Mkuu wa gereza na uongozi mzima wa gereza la Loliondo wameishukuru sana THRDC na NGOLAC kwa msaada huo wa magodoro pamoja na vitu vingine vilivyoletwa na mashirika hayo.
SP Osindi atoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa mashirika haya kusaidia wafungwa, kwa sababu wana mahitaji kadhaa.
Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa amepongeza uongozi wa gereza la Loliondo kwa hali nzuri na ya usafi kwenye gereza hilo.
Ole Ngurumwa ambaye ni mzaliwa wa Ngorongoro alisema Mazingira ya gereza hilo ni mazuri na rafiki kwa wafungwa kupata ujuzi wa kazi mbalimbali kama vile utunzaji wa bustani, ufundi seremala, ujenzi na nyingine.
Alisema msaada huo umetolewa ikiwa ni moja ya jitihada za kuboresha na kuimarisha haki za binadamu, kupitia misingi ya haki jinai nchini
"Natoan wito kwa mashirika na wadau wengine kujitahidi kuimarisha haki jinai nchini kwa njia ya utoaji huduma kwa wafungwa na mahabusu"alisema
Mwisho.
No comments:
Post a Comment