Na Mwandishi Wetu
maipacarusha20@gmail.com
Mnada wa nne wa Korosho uliofanyika Tarehe 12 Novemba 2024 Wilayani ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma kupitia Chama kikuu cha Ushirika TAMCU, umepelekea kuuzwa kwa Tani 4,837 kwa bei ya Wastani ya Shilingi 3,290/=
Mnada huo ambao umesimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania TMX, umefanyiaka katika Kijiji cha Ligoma Kata ya Ligoma Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma na kuhudhuriwa na wakulima wa Korosho huku bei ya chini ikiwa ni shilingi 3,200/=
Afisa Mwandamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania- TMX Bi. Ezelin Mboma, ameeleza kuwa bei za Korosho katika Mkoa wa Ruvuma zimeendelea kuimarika kutokana na wanunuzi wanaoendelea kujitokeza.
"Bei ni nzuri na wakulima wanaendelea kuulewa mfumo huu wa kuendesha minada kidijitali ambao unawapa nafasi ya kushuhudia kila kinachoendelea kutoka kwa wanunuzi" amesema
Katika mnada huo, Chama Kikuu cha Ushirika TAMCU, kilipeleka sokoni kiasi cha Tani 4,837 sawa na Kilo 4,837,819 ambazo zote zimenunuliwa.
Mohamed Bakari, Mkulima wa kijiji cha Ligoma ameeleza kufurahishwa na bei za msimu wa mwaka huu, ambazo amesema zimechangiwa na uwazi uliopo kwenye minada inayosimamiwa na TMX.
Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Bi.Shauri Mokiwa amezungimzia kuendelea kuimarika kwa bei kuwa kumetokana na mazingira mazuri ya minada ya msimu 2024/2025 ambayo yamewekwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wanaoshirika katika minada ya Korosho.
Mussa Athumani Manjaule Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika TAMCU, amewasisitiza wakulima kuzingatia ubora katika Korosho zao, ili zizidi kufanya vizuri pale zinapopelekwa sokoni.
No comments:
Post a Comment