Na: Epifania Magingo,Manyara
maipacarusha20@gmail.com
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Samweli Warioba Gunzar amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kwa makosa mawili la matumizi mabaya ya madaraka na kutotimiza wajibu wa kisheria ambapo ni kinyume cha sheria.
Akisoma shauri hilo Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Wilaya ya Simanjiro Wakili Faustin Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu mfawidhi wa Wilaya ya Simanjiro Charles Uisso amesema mshitakuwa katika nyakati tofauti akiwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro alitoa zabuni ya ukusanyaji wa mapato ya soko la mnada wa Orkesumet kwa mwananchi aitwaye Elias Lazaro Tipiliti bila ya kuwepo kwa tangazo la zabuni na bila ya zabuni hiyo kushindanishwa.
Mwendesha Mashtaka Faustin Mushi amesema mshtakiwa amekana makosa yote mawili na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana kwa kupeleka wadhamini wawili ambao ni watumishi wa umma pamoja na kusaini bondi ya shilling million mbili.
Imeelezwa kuwa, kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Februari 11 mwaka huu, kwaajili ya kusikilizwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.
No comments:
Post a Comment