Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima |
Katibu tawala mkoa wa Morogoro Mussa Ali Mussa |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
KIASI Cha Sh Bil 11.5 zimeidhinishwa na Serikali na zinatarajiwa kutolewa kwa vikundi 467 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyokidhi vigezo vya kupata mkopo wa asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Afisa Maendeleo ya jamii mkoa wa Morogoro Dickson Makoba alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya hali ya utoaji mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10.
Makoba alisema hadi kufikia Desemba 31 mwaka 2024 halmashauri zote za mkoa wa Morogoro zimekamilisha awamu ya kwanza ya taratibu za utoaji mkopo kwa vikundi vya wanawake(293), vijana(147) na watu wenye ulemavu(38).
"Watu wenye ulemavu tu watapatiwa kiasi cha shilingi milioni 849.1,"alisema.
Afisa huyo alisema kuanzia mwezi Aprili 2023 Serikali ilisitisha utoaji mikopo inayotokana na asilimia kumi mapato ya ndani ya halmashauri ili kutengeneza utaratibu mzuri utakaowezesha wanufaika kukopa na kurejesha kwa wakati.
Alisema ili kuondokana na changamoto ya vikundi kutorejesha mikopo wanayopewa na Serikali imefanya mabadiliko katika kanuni na muongozo wa utoaji mikopo kwa vikundi hivyo.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima alisisitiza kutokuwa na urasimu katika utoaji mikopo hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hiyo.
Pia alisisitiza kuwa fedha hizo kwa sasa zitakuwa na usimamizi na ufuatiliaji wa hali ya juu kutokana na matumizi mabaya ya vikundi hewa yaliotokea hapo awali .
"Wapo watu walitengeneza vikundi hewa wakachukua fedha na kisha mikopo haikulipwa, ndipo Rais Samia Hassan Suluhu akasitisha kwa muda" alisema.
Naye katibu tawala mkoa wa Morogoro Dk Mussa Ali Mussa akazitaka halmashauri za wilaya kuunga mkono vikundi vinavyopewa mikopo kwa kununua bidhaa zao.
"Halmashauri ziwaelimishe wenye vikundi vinavyoomba mikopo viwe vinazalisha, vikundi vingi havizalishi ndio maana vibashindwa kurejesha mikopo" alisema.
Mwenyekiti wa Chama Cha Ualibino(TAS)Morogoro Hassan Mkazi alisema ipo changamoto ya watu wenye ulemavu kutokana mfumo wa kieletroniki ya kuomba mkopo hususani kwa wenye uoni hafifu, wasiosikia na wasioona .
Mwisho.
No comments:
Post a Comment