Na Mwandishi Wetu Maipac
maipacarusha20@gmail.com
Baadhi ya Wananchi wanaoendelea kujitokeza kupata msaada wa Kisheria kutoka Halmashauri za Wilaya ya Mtwara, wameeleza kufurahishwa na msaada wa kisheria wanaoupata kupitia kamapeni ya Mama Samia Legal Aid.
Kampeni hiyo leo tarehe 26 Januari 2025 imewafikia Wananchi katika Vijiji vya Mnyija, Libobe na Ming'wena Halmashauri ya Mtwara, na wale wa maeneo ya Mtawanya na Mangamba Mtwara Manispaa, huku watendaji wakipokea kero za wananchi na kutoa ushauri wa Kisheria.
Wakili Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Emmanuel Mbega ambaye ni Mratibu wa Samia Legal Aid Campaign Mkoa wa Mtwara, amesema huduma za msaada wa kisheria zinaendelea kutolewa katika Halmashauri Tisa za Mkoa wa Mtwara, na muitikio wa Wananchi ni Mkubwa.
"Wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanaendelea kunufaika na huduma hii, mimi kama mratibu napokea taarifa za maendeleo kutoka Halmashauri zote Tisa kila siku" amesema Wakili Mbega
"Nimetembelea mwenyewe kuona kazi inavyoendelea katika Halmashauri mbili za Wilaya ya Mtwara ambapo nyie wenyewe qaandishi ni mashihidi mmeona namna ambavyo wananchi ambao mezungumza nao wanafurahia huduma hii ambayo wanakiri kuwa walikuwa wanaihitaji kwa muda mrefu" ameeleza Wakili Mbega.
Akizungumza kwa niaba ya Wanachi wenzake Bi.Farida Ismail Mkazi wa Mtawanya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani amewahimiza wananchi wengine kujitokeza ili kupata huduma za msaada wa kisheria katika sekta mbalimbali.
"Tunamshukuru sana Mama Samia kwa kutuletea huduma hii maana inagusa watu wenye matatizo katika ngazi ya chini, sisi wananchi tuna changamoto nyingi ambazo hatuwezi kuzitatua bila kuwa na hela, lakini kwa hii huduma ya Mama Samia tunahudumiwa bure" amesema Farida.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa Mkoa wa Mtwara, ilizinduliwa rasmi Januari 24,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala na inaendelea kuwafikia wananchi katika Halmashauri zote, huku ikitarajiwa kuhitimishwa Februari 02, 2025.
No comments:
Post a Comment