Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Ofisi ya Kiunganishi ya TANAPA, Dar es Salaam Neema Mollel |
Na: Mwandishi wetu,MAIPAC
maipacarusha@gmail.com
Shirika la hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) limeeleza mafanikio makubwa yanaendelea kupatikana katika sekta ya Utalii kutokana na kazi kubwa na nzuri ya kutangaza vivutio ambayo inaendelea.
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji ameyasema hayo leo tarehe 01, Februari 2025 katika kikao kazi na Maafisa na Askari Uhifadhi waliopo katika Ofisi Kiunganishi ya TANAPA iliyopo jijini, Dar es Salaam pamoja na Nyumba Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni.
Kuji amewataka watanzania na wafanyakazi wa TANAPA kuendelea kujipanga vyema kupokea maelfu ya watalii nchini kwa kutoa huduma bora.
Kupitia kikao kazi hicho Kamishna Kuji aliipongeza Ofisi Kiunganishi pamoja na Nyumba Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere kwa juhudi kubwa zinazofanyika katika kujitangaza na kuwataka kuongeza Ari na Kasi zaidi katika utangazaji na utoaji wa taarifa katika ofisi mbalimbali na ili kupeleka elimu ya Uhifadhi na Utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa.
“Jana kupitia uzinduzi wa takwimu za utalii na mapato maarufu kama “T 506 USD” tulishudia mapinduzi makubwa yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na filamu ya “Tanzania :The Royal Tour” na “Amazing Tanzania” mapato tunayoingiza sasa TANAPA ni “Amazing” kama ilivyo filamu aliyocheza Mhe.Rais ambapo mapato yaliongezeka kutoka mapato ya billioni 57 wakati wa janga la COVID -19 TANAPA ikafikisha mapato billioni 411, kwa mwaka wa fedha 2023/24 na mpaka jana kwa mwaka wa fedha 2024/25 TANAPA imekusanya billioni 365 ikiwa ni miezi saba tu ya makusanyo” alisema Kamishna Kuji.
“Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasaan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshafanya sehemu yake ni jukumu letu watendaji tuliopo chini yake kuendeleza Ari na Kasi kubwa aliyoanza nayo katika kunadi Utalii wetu na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo yote ya Hifadhi za Taifa niwatake mkatekeleze hili kwa nguvu kubwa ili kufikia malengo ya Serikali iliyojiwekea” Alisema
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Ofisi ya Kiunganishi ya TANAPA, Dar es Salaam Neema Mollel, alimshukuru Kamishna wa Uhifadhi kwa uongozi makini na katika kutoa maelekezo yenye mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa TANAPA inatekeleza majukumu yake ipasavyo na kuahidi kuendeleza Ari na Kasi katika kusimamia majukumu kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Ofisi za Kiunganishi za TANAPA ni maalum katika kuendelea kutangaza vivutio vya Utali, kuhamasisha watalii kutembelea maeneo ya vivutio pamoja na kunadi fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo ya Hifadhi za Taifa nchini.
Kamishna Kuji anaendelea na ziara yake ya kikazi katika hifadhi za kanda ya mashariki.
No comments:
Post a Comment