Na: Mussa Juma,maipac
maipacarusha@gmail.com
Manyoni. Kampuni ya uwindaji wa kitalii ya EBN kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) imetoa msaada wa viti mwendo 49 kusaidia wananchi wenye uhitaji wilayani Manyoni, mkoa wa Singida.
Viti hivyo vinathamani ya sh 39.2 milioni na vimetolewa na kampuni hiyo ambayo imewekeza shughuli za utaliii katika pori la akiba la kizigo ,Itigi wilayani Manyoni.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa viti mwendo 25 kwa Wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya msingi Sayuni wilaya ya Manyoni, Meneja wa EBN Eric Nyman alisema wametoa msaada huo kuthamini mchango wa jamii inayowazunguka katika utunzaji wa mazingira.
"Sisi tunajitahidi kutunza mazingira pia kuendelea kushirikiana na jamii na wahifadhi kutunza mazingira na wanyamapori lakini pia tunathamini mchango wa wananchi katika uhifadhi"alisema
Alisema EBN itaendelea kushirikiana na kusaidia jamii katika katika mambo ya maendeleo.
Mkuu wa pori la akiba la Kigosi wa TAWA, Gasaya Ogosi alisema msaada huo ni miongoni mwa mikakati ya TAWA na EBN kuhakikisha wananchi wananufaika na uhifadhi wa mazingira na wanyamapori katika maeneo yao.
" TAWA inalenga kuhakikisha faida za uhifadhi zinaenda pia kwa jamii ambayo inazunguka mapori ya akiba kwani pia kuna mradi mwingine wa kudhamini masomo kwa wanafunzi kutoka kaya masikini ambao unaendelea"alisema
Alisema katika msaada huo, wananchi wenye uhitaji tarafa ya Nkonko imepata viti mwendo 20, Kituo cha afya Nkonko viti 4 kusaidia wagonjwa wanaofikishwa na shule ya Sayuni viti mwendo 25.
Mkuu wa TAWA Kanda ya Kati, Herman Nyanda aliwaomba wananchi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi ikiwepo kupinga matukio ya ujangili na uharibifu wa mazingira ili waendelee kunufaika na uhifadhi.
Akizungumza baada kukabidhiwa viti hivyo na kuvikabidhi kwa walengwa mkuu wa wilaya ya Manyoni, Dk Vincenti Mashinji alishukuru kampuni ya EBN na TAWA kwa msaada huo.
Hata hivyo, Dk Mashinji aliwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na alitangaza kupiga marufuku ufyekaji vichaka ya mapori kwa ajili ya mashamba bila kuwa na vibali vya mamlaka ya misitu TFS.
"Vichaka katika mapori yetu ya Itigi vinasifika kwa kuzalisha asali bora duniani lakini pia ndio mazalia ya Tembo hivyo lazina tutunze maeneo haya"alisema.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment