📌 Hospitali ya Shirika la Mzinga kikosi cha Jeshi Mazao yaanza matengenezo ya viungo bandia
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ ni sehemu muhimu kwa Mustakabali wa uhai wa taifa na kwa namna nyingi na si kwa ajili ya ulinzi pekee bali ni ushiriki wa mfano kwa masuala ya kijamii.
Alisema hayo wakati wa kukabidhi mguu bandia kwa Mzee Jackso Mwakalinga(75) mwenye changamoto ya ulemavu wa mguu katika zoezi lililofanyika katika ofisi ya mkuu huyo wa mkoa.
Malima alisema, mwezi Agosti mwaka jana 2024 wakati hospitali ya shirika la Mzinga iliyo chini ya shirika la Mzinga na kikosi cha Mazao wakitoa huduma ya matibabu bure kwa wananchi wa Morogoro kwenye viwanja vya sekondari ya Morogoro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi la wananchi wa Tanzania alikutana na Mzee Jackson aliyemuomba amsaidie kupata mguu bandia ndipo Malima alipoahidi kugharamia matengenezo yake.
Baada ya maombi hayo, Malima alielekeza uongozi wa Shirika la Mzinga na kikosi cha Jeshi Mazao walioahidi kuanza kutoa huduma za viungo tiba na vifaa saidizi katika Hospitali yake kufanya matengenezo ya mguu huo bandia ambao angeugharamia.
Mkuu huyo wa Mkoa baada ya kukabidhi mguu huo kwa Mzee Jackson alisema kwa sasa wananchi wenye uhitaji wa huduma wa viungo bandia badala ya kukimbilia maeneo mengine ya mbali yenye huduma kama hizo ni vyema wakatumia uwekezaji uliofanywa na JWTZ katika utoaji huduma hiyo kupata huduma hiyo mjini Morogoro.
“Mzee Mwakalinga umekuwa kama muonyesha njia katika hili na kwamba watu wa morogoro ni wanufaika wa uwekezji uliofanywa na jeshi la wananchi katika kuboresha wa afya hasa ukizingatia mwaka 1976 Hospitali hii ilikuwa zahanati ya kutoa huduma kwa watu wachache maofisa wa serikali na sasa ni Hospitali kubwa inayotoa huduma,”alisema.
Akamuelekeza mganga mkuu wa Mkoa kushirikiana na wataalamu wake kuangalia namna ambavyo Hospitali ya Mzinga inaweza kushirikiana na Hospitali nyingine ndani na nje ya Mkoa wa Morogoro kwaajili ya huduma hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea mguu huo bandia, Jackson Mwakalinga(75)alisema awali alichomwa na mfupa wenye ncha kali nyumbani kwake na mguu kuanza kuuma na kutokea kidonda kisichopona kutokana na yeye kusumbuliwa pia na ugonjwa wa sukari uliosababisha kukatwa juu ya goti la mguu wake wa kushoto mwaka 2006.
Miaka 19 tangu kukatwa kwa mguu huo, mzee Jackson ambaye alikuwa dereva wa Lori akiwa anasafiri nchi za nje ikiwemo Burundi,alisema tangu hapo amekuwa akihangaika kupata mguu bandia bila mafanikio ambapo ameenda makanisani na maeneo mengine kuomba msaada.
“Mwanzo nilivyojichoma nilienda kwenye kihospitali cha binafsi kidonda kikawa kinachimbika mpaka mfupa kuonekana,Nilikatwa mguu katika Hospitali ya taifa Muhimbili mwaka huo 2006,”alisema.
Meneja mkuu , Shirika la Mzinga na Mkuu wa kikosi Mazao Brigedia Jenerali Seif Athuman Hamisi
Alisema Mguu huo umetengenezwa kwa kiwango cha hali ya juu kilichozingatia vigezo na viwango na alieleza kuwa mguu huo bandia imelipiwa kiasi cha sh milioni 2.1, ambapo ghalama ya mguu huo ni sh milioni 2.5.
Aidha akasema hospitali ya Mzinga ina madaktari bingwa sita(6), na alitaja huduma zinzotolewa hospitali hapo kuwa ni huduma za matibabu ya kawaida na huduma za kibingwa ikiwemo kwenye magonjwa ya dharura, wanawake,njia ya mkojo, mifupa,magonjwa ya ndani na sasa wameanza kutoa huduma ya viungo tiba na vifaa saidizi.
Hosptalii ya shirika la Mzinga kitengo cha viungo tiba na vifaa saidizi inatoa huduma za viungo tiba kwa wenye ulemavu wa kupoteza viungo ikiwemo ajali,Magonjwa yasiyoambukiza na ulemavu wa viungo wa kuzaliwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment