Takukuru Tanga yaokoa sh 76 Milioni - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 6 February 2025

Takukuru Tanga yaokoa sh 76 Milioni






Na: Burhani Yakub,Tanga.


maipacarusha20@gmail.com 


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeokoa jumla ya sh 76 milioni za Serikali ambazo zilikuwa zimehujumiwa katika Wilaya tatu za mkoa wa Tanga.


Kiasi hicho cha Shilingi 76,048,459.21 ziliamuliwa na Mahakama kurejeshwa katika Halmashauri za Wilaya ya Kilindi,Tanga na Korogwe kufuatia watumishi wake kutoziwasilisha sehemu husika baada ya kuzikusanya na kuzitumia kwa manufaa yao binafsi.


Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kuanzia Oktoba Hadi Disemba 2024 iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah (pichani ) ni kuwa fedha hizo zimerejeshwa Serikalini baada ya Jamhuri kushinda kesi katika mahakama mbalimbali mkoani hapa.


Amesema Wilaya ya Kilindi Jamhuri ilifungua kesi za uhujumu uchumi namba 13/2023,11/2023 na 06/2024 dhidi ya watumishi ambao walishtakiwa kwa ubadhirifu kufuatia kutowasilisha sh 58,678,780 ambazo ni mapato ya Serikali yaliyokusanywa kwa mfumo wa POS na kuzitumia kwa manufaa yao pasipo kuwasilisha sehemu husika kwa taratibu zilizowekwa.


Wilaya ya Korogwe jumla ya sh 9,198,045.31 ambazo ni mapato ya Serikali yalikusanywa kwa mfumo wa POS zilirejeshwa kwa amri ya mahakama kufuatia Jamhuri kushinda kesi za uhujumu uchumi namba 09/2023 na 10/2023.


Amesema Jiji la Tanga Jamhuri ilishinda kesi za uhujumu uchumi namba 16558/2025 na 07/2023 jumla ya sh 3,171,633.9 zilizofanyiwa ubadhirifu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na sh 5,000,000 ya mikopo ya asilimia 10 Kwa ajili ya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.


Mkuu huyo wa Takukuru amesema mbali ya kurejeshwa fedha hizo zilizohujiwa kwa amri ya mahakama watumishi waliohusika pia wamepewa adhabu nyingine.


"Takukuru inatoa onyo kali kwa wote wanaofikiria kufanya hujuma ya aina yoyote katika matumizi ya raslimali za umma...tunawaasa waache fikra hizo na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma"amesema Ndwatah.


Amesema katika kipindi hicho takukuru iliendelea na ufuatiliaji wa miradi 42 ya maendeleo yenye thamani ya sh sh 15,441,281,669 huku miradi minne yenye thamani ya sh 248 Milioni ni katika sekta ya afya, miradi 34 yenye thamani ya sh 3,727,385,910 sekta ya elimu, miradi mitatu yenye thamani ya sh 5,390,895,759 sekta ya maji na mradi mmoja wenye thamani ya sh 6,075,000,000 katika sekta ya utawala.


"Kati ya miradi hiyo iliyofanyiwa ukaguzi,jumla ya miradi 24 yenye thamani ya sh 13,978,645,106 ilikuwa na mapungufu ambayo baada ya kubainika wahusika walijulishwa na kushauriwa ambapo dosari zilifznyiwa marekebisho"amesema Ndwatah


MWISHO

No comments: