SHUHUDIA MAAJABU KIJIJI CHA NYUKI NCHINI KINAINGIZA MAMILIONI YA SHILINGI, WATALII NA WANAFUNZI WATEMBELEA KUJIFUNZA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 25 February 2023

SHUHUDIA MAAJABU KIJIJI CHA NYUKI NCHINI KINAINGIZA MAMILIONI YA SHILINGI, WATALII NA WANAFUNZI WATEMBELEA KUJIFUNZA



Moja ya mizinga ya nyuki inayopatikana kijijini hapo

mtaalam akirina asali toka katika mzinga wa nyuki

wataalam wakiwa katika kiwanda cha kuchakata asali kwa ajili ya kumfikia mlaji
 


NA: Mwandishi wetu, Maipac 
 
Shirika la Chakula Duniani (FAO) linaeleza kuwa,Tanzania ni nchi ya pili kwa ufugaji nyuki barani Afrika baada ya Ethiopia.

Ubunifu na ufugaji wa nyuki katika kijiji cha nyuki kilichopo mkoani Singida  kilichoanzishwa rasmi mwaka 2008 na kuzinduliwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda unathibitisha kuwa Tanzania tunaweza kuwa miongoni mwa nchi vinara duniani kwa uzalishaji mazao ya nyuki na mazao yake na kuuza katika masoko ya kimataifa.

Kijiji hiki kipo takribani kilomita 12 kutoka Singida mjini kuelekea barabara kuu ya Dodoma na kikiwa na jumla ya ekari 45,000 ambapo zipo katika Kata za Kisaki, Ikungi, Iglansoni, Itigi Mkoani Singida na Kata ya Uyui iliyopo mkoani Tabora.
 
 
Mwanzilishi wa mradi huu ni Philemon Josephat Kiemi, almaarufu "Kiemi" ambaye ni mhitimu wa shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) akibobea katika masuala ya ufugaji nyuki kibiashara na kilimo .

Kiemi anasema ameweza kutoa ajira za watu 114 ambao wana utalaam wa fani mbalimbali kuhusiana na Kilimo, biashara na ufugaji wa nyuki kibiashara.

Anasema licha ya kuwa na mradi wa nyuki katika eneo hilo pia amekuwa akipokea watalii na watu mbali mbali kujifunza ufugaji nyuki na faida zake lakini pia kushuhudia uhifadhi wa mazingira na kilimo rafiki na ufugaji nyuki.
 

Kiemi anasema alikuwa na ndoto ya kufanya jambo la kipekee katika ufugaji nyuki na ndipo aliamua kwanza kujiendeleza na kupata elimu chuo kikuu cha kilimo Sokoine na kabla ya hapo alisoma Hebrew University of Jerusalem.

Mazao ambayo yanapatikana katika kijiji hicho kwa sasa ni asali asilia (Organic Honey)hii asali iliyopewa jina la "Singida Asali" au "IFONEO" akiwa na upekee kutokana na utamu wake na harufi nzuri ambayo inatokana na misitu asili ya singida.
 
 
Anasema pia katika kijiji hicho wanazalisha bidhaa ya nyuki iliyopewa jina la vumbi la singida ambayo inaimarisha kinga ya mwili, kuongeza vitamini na protini mwilini lakini pia husaidia kukomesha tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.
 

Katika kijiji hiki pia wanazalisha mishumaa inayotokana na nyuki; huu ni Mshumaa ambao ni maalumu kwa kuwasha chumbani kwa ajili ya Kusafisha hewa, kutoa Mwanga na kutoa harufu nzuri na pia sehemu ya matibabu ya macho.


Kiemi anasema pia wanazalisha sumu ya nyuki (Bee venom) ambayo inasaidia kuongeza kinga ya mwili wa Binadamu kupambana na magonjwa ikiwepo Kansa na kufubaza virusi vya UKIMWI huku ikiiacha seli hai zikiwa salama.
Anasema wanazalisha Gundi ya nyuki hii ni bidhaa ya nyuki ambayo ni inazuia Bacteria, fangazi na pia hutumika kama kipodozi na katika matumizi ya kitabibu

Pia katika kijiji hicho wanazalisha Maziwa wa nyuki (Royal jelly) hii ni bidhaa ambayo humfanya mtu asizeeke mapema kwani huunganisha mwili na kuupa uimara.

“Hii ni bidhaa ya chakula pekee cha malkia wa nyuki kwenye Mzinga ambapo malkia akila huishi miaka 3-5 na nyuki wengine wasiokula hichi chakula huishi siku 55-60 toka kwenye yai”anasema

Anasema maziwa haya yanawavuta wanasayansi wengi kufanya utafiti uliopelekea binadamu wanaotumia zao hili kuchelewa kuzeeka.

Kiemi anasema wanazalisha pia Supu ya nyuki (BEE BROOD) zao ambalo linatokana na watoto wa nyuki lina protini nyingi. Wazee wengi na wavunaji wa asali wanatafuna masega yakiwa na matoto yale pamoja.

“Hii kwa historia inasadikika wanaokula hivi wawaumwi maradhi mbalimbali mara kwa mara”anasema

Mkurugenzi huyo anasema katika kijiji hicho, pia wanatoa elimu ya ufugaji nyuki na huduma nyingine zitokanazo na nyuki ikiwepo utengenezaji wa Mizinga, Mitego ya chavua ya nyuki na mavazi ya kujikinga na nyuki .
 
“pia tunatoa Mafunzo ya Ufugaji wa nyuki Kibiashara kwa Vitendo na watu wengi wanafika hapa kujifunza na kwa anataka maelezo zaidi awasiliane nasi ”anasema

 

     Aelezea maajabu ya kijiji hicho.

Akielezea kijiji hicho, ndugu Suphian Juma ambaye ni Mwanasiasa  na Mdau  wa masuala ya Utalii, alipoenda kupata mapumziko kijijini hapo ,anasema ameshangazwa na ubunifu mkubwa katika kijiji hicho ambao licha ya kuzalisha mazao ya nyuki pia kuna pori kubwa la miti ya asili yenye urefu wa wastani kuna nyumba kadhaa za rangi ya karoti zikijengwa mbalimbali huku umeme na miundo mbinu ya maji ikisambazwa huko ndani kikamilifu.

Juma anasema katika kijiji hicho kila nyumba ina matumizi yake, zipo nyumba za Makazi, ofisi, viwanda na kadhalika jambo ambalo limefanywa na ubunifu mkubwa.

“Hii ni Uwekezaji unastahili kuitwa na kubeba maantiki ya neno "kijiji" kwa kuzingatia tafsiri ya kuona mwingiliano wa shughuli za ufugaji wa nyuki, Makazi ya Watu (wafanyakazi), miundo mbinu ya huduma za kijamii, miti asilia, ndege, wanyama kama digidigi, Sungura na kadhalika”anasema.

“Baada ya kuelezwa mengi juu ya mradi huu nilipelekwa kiwanda cha kutengeneza mizinga ambapo nilijionea vijana wengi wa kike na wa kiume wakitengeneza mizinga mizuri sana, kuanzia kwenye muonekano hadi kwenye uimara “anasema

 
Anasema kijiji hicho kimeweza kuwa na uwezo wa kufunga mashine za kisasa kutengeneza asali na mazao mengine jambo ambalo ni kivutio kikubwa.

“kijiji hicho ni mfano tosha kwa kile ambacho amekuwa akihimiza Rais Samia suluhu vijana kujitokeza kujiajiri na serikali itaendelea kuwapa mazingira mazuri ya kufikia malengo yao”anasema Suphian

Juma anatoa wito kwa watanzania kutoka maeneo mbalimbali na watalii kufika katika kituo kijiji hicho, kuona mazao ya nyuki lakini pia kujifunza ufugaji nyuki wa kisasa na kibiashara.

Rehema Nkuwi anasema katika kijiji hicho, kuna mengi ya kujifunza ikiwepo utunzwaji mzuri wa mazingira.

“hapa tunajifunza uvunaji wa asali bila kuathiri maisha ya nyuki lakini pia jinsi ya kuchuja asali na kuihifadhi ili isiharibike”anasema

Nkuwi anasema huduma ambazo zinatolewa ,katika kijiji hicho, ikiwepo maeneo ya kulala wageni, vyakula na mahitaji mengine inaonesha vijana wa kitanzania wakipewa fursa wanaweza kufanya maajabu.

Hiki ndicho kijiji cha nyuki ambacho kina maajabu ya aina yake ikiwepo ubunifu katika uandaaji mazao ya nyuki, uvunaji wa nyuki na uandaaji ya mashamba ya nyuki na kuwa eneo la kivutio cha utalii. 

No comments: