NAIBU WAZIRI MASANJA ATATUA MIGOGORO YA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI YA NGORONGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 25 February 2023

NAIBU WAZIRI MASANJA ATATUA MIGOGORO YA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI YA NGORONGORO

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii   Mary Masanja akizungumza na wakazi wa VIJIJI vinavyozunguka hifadhi 


 




Na Mwandishi wetu, Maipac 

maipacarusha20@gmail.com

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) amefanya ziara katika vijiji vinavyozunguka eneo la hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara.


Ziara hiyo imelenga kutatua changamoto ya mipaka kati ya Kijiji cha Lositete na Bugeri vilivyopo Wilayani Karatu ambapo awali kulikuwa na changamoto ya mipaka iliyopelekea baadhi ya wananchi kuingiza mifugo Hifadhini na kulima kwenye mipaka ya hifadhi na kusababisha migongano kati ya Wanyamapori na wananchi.


“Kulikuwa na mgogoro ya kimipaka kati ya Kijiji cha Lositete na Hifadhi ya Ngorongoro,  wananchi wanavuka mipaka na kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi.  


Nafurahi kusikia kuwa wahifadhi wa Ngorongoro mumewaelimisha wananchi kwa kufanya vikao vya maridhiano na sasa kwa ridhaa yao wamekubali kutoingiza mifugo hifadhini,  Ilindeni hifadhi hii ambayo manufaa yake ni makubwa na nyie ni sehemu ya wanufaika” amesisitiza Mhe Masanja.


Akizungumzia kuhusu mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Bugeri na Hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara mhe Masanja amesema Serikali kupitia kamati ya mawaziri 8 imetoa maelekezo kwa wananchi waliovamia mipaka kutambuliwa, kufanyiwa tathmini na kulipwa fidia ili kupisha eneo walilovamia kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.


Akiwa katika Kijiji cha Lositete Mhe. Masanja ameuelekeza uongozi wa NCAA kuendeleza programu za ujirani mwema na kutoa elimu ya Uhifadhi shirikishi kwa wananchi wa Tarafa ya Mbulumbulu wanaopakana na msitu wa nyanda za juu kaskazini ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.



Katika kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri, Naibu Kamishna wa Uhifadhi- NCAA Needpeace Wambuya, amebainisha kuwa katika kuimarisha ulinzi shirikishi NCAA imekuwa ikitoa miti kwa wanavijiji kupanda katika maeneo yao na kudumisha elimu ya uhifadhi sambamba na kuongeza askari wa doria na vituo vya askari ili kuzuia wanyama waharibifu wanaoingia kwenye mashamba na makazi ya Wananchi


Ameahidi kuwa uongozi wa NCAA utaendelea kushirikiana na jamii hasa katika ulinzi kwa kutoa elimu ya uhifadhi na kutumia vijana waliosomea uaskari katika  vijiji ili kusadia kufukuza Wanyama katika wanaoingia maeneo ya wananchi.


Wambuya  ameongeza kuwa kadri bajeti inavyoruhusu, NCAA itaendelea  kutoa miradi ya huduma za jamii ili kusaidia wananchi wa kijiji hicho ambao ni sehemu ya wa wadau wa uhifadhi.




Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba na Diwani wa kata ya Mbulumbulu Mhe. Elias Simba wameeleza kuwa, kutatuliwa kwa migororo ya Mipaka kati ya Hifadhi na wananchi imerejesha imani kwa jamii na kuahidi kushirikiana na NCAA kutatua changamoto zitakazojitokeza kati ya wananchi na wanyamapori ili kulinda hifadhi hiyo ambayo inasaidia wananchi kupata vyanzo vya maji na mvua kwa ajili ya mazao ya chakula.

No comments: