Shoroba 41 hatarini kufungwa, Dc aonya wanaochochea Migogoro maeneo ya hifadhi. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations
Saturday 9 December 2023

Shoroba 41 hatarini kufungwa, Dc aonya wanaochochea Migogoro maeneo ya hifadhi.Na: Mwandishi wetu, Arusha.


maipacarusha20@gmail.com


Wakati Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) ikieleza mapito ya wanyama (shoroba) 41 yapo hatarini kufungwa kutokana na ongezeko la shughuli za kibinaadamu, Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange ameonya viongozi wa vijiji wanaohamasisha uvamizi wa maeneo hayo.


Maeneo ya mapito ya Wanyama ni muhimu katika Utalii, uhifadhi na kibaiolojia kwa Wanyamapori kwani ndio yanatumiwa na wanyama kutoka eneo moja kwenda jingine kutafuta malisho ,uzao mpya na kujilinda na magonjwa.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Utafiti wa TAWIRI Dk. Julius Keyyu alisema maeneo ya shoroba 41 nchini, ikiwepo eneo muhimu la shoroba ya kwa kuchinja wilaya ya Babati yapo hatarini.

Dkt. Keyyu akizungumza na waandishi wa habari 

Dk Keyyu alisema, kuna Shoroba 61 katika maeneo mbali mbali nchini, 20 tayari zimejifunga na hivyo bila hatua za haraka kuchukuliwa tatizo litakuwa kubwa zaidi.


"Jambo ambalo Tunaliomba ni kulindwa Shoroba hizi na vijiji, kwa kuhakikisha vijiji vinakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, kwa kutenga maeneo ya wanyamapori, maeneo ya makazi, kilimo na shughuli nyingine za kijamii"alisema


Alisema hivi sasa shoroba muhimu zipo hatarini, ikiwepo shoroba ya kwa kuchinja, ambayo ipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara.


"Ambacho hadi sasa kinasaidia kutofungwa kabisa Shoroba hii ni uwepo wa hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge na tunawashukuru sana walioanzisha hifadhi hii kwani bila wao nadhani hali ingekuwa mbaya zaidi"alisema

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange

Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange, akizungumzia jitihada za kulinda uhifadhi ikiwepo mapito ya wanyamapori, aliwataka viongozi wa vijiji vinavyounda Burunge WMA wanaochochea migogoro kuacha mara moja.


Twange akizungumza na viongozi wa kijiji cha vilimatatu moja ya vijiji vinavyounda Burunge WMA, alisema serikali inajua kuna baadhi ya viongozi waliopo madaraka na wastaafu, wanachochea migogoro katika eneo hilo kupinga shoroba kwa manufaa yao.


"Wewe kama kiongozi unaona huwezi kusimamia mipango ya serikali kuendeleza uhifadhi na kulinda Shoroba basi bora uachie ngazi lakini serikali lazima itachukuwa hatua kwa wachochezi wote"alisema.


 Baadhi ya Wananchi wa Kijiji Cha Vilima vitatu wakiwa wamefunga ofisi ya kijiji hicho wakipinga ushoroba 


Katika kijiji hicho, hivi karibuni wananchi waliandamana na kufunga ofisi za serikali ya kijiji cha vilima vitatu, wakipinga kuwekwa alama za shoroba katika maeneo yao.


Waziri wa maliasili na Utalii, Angella Kairuki, akizungumza katika kongamano la 14 la Wanasayansi, lililoandaliwa na taasisi ya wanyamapori (TAWIRI) alitaka kulindwa kwa maeneo 41 ya Shoroba nchini ili kuendeleza uhifadhi na Utalii.


Alisema Shoroba 20 tayari zimejifunza kabisa na hivyo serikali inafikiria kuziondoa katika orodha na hivyo kubaki Shoroba 41 tu katika maeneo mbali mbali nchini

No comments: