DIWANI LUKA AMUOMBA CHONGOLO HOSPITALI, MAJI NA MJI WA MIRERANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 11 March 2023

DIWANI LUKA AMUOMBA CHONGOLO HOSPITALI, MAJI NA MJI WA MIRERANI

Katibu wa CCM Daniel Chongolo akisalimiana na Diwani wa Kata ya Endiamtu Lucas Chimbason Zacharia

 

Na Mwandishi wetu, Mirerani 

maipacarusha20@gmail.com

DIWANI wa Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia Agwiso amemlilia Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ili wakazi wa mji mdogo wa Mirerani wapate maji, kituo cha afya Mirerani kipandishwe hadhi kuwa hospitali na Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani kuwa Mji kamili.


Kutokana na hali hiyo Diwani Luka amelazimika kumpigia magoti Katibu Mkuu CCM Daniel Chongolo ili kuomba huduma hizo zifanikishwe kwani CCM ndiyo inayounda Serikali.


 Diwani Luka amesema kituo cha afya Mirerani kilichopo Kata ya Endiamtu kinapaswa kupandisha hadhi kuwa hospitali kwani kinahudumia wagonjwa wa mikoa mitatu jirani ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.


Amesema kituo cha afya Mirerani kwa siku kinahudumia wagongwa 260 hadi 300 wanaotoka kwenye Wilaya za Simanjiro Mkoani Manyara, Arumeru Mkoani Arusha na Hai Mkoani Kilimanjaro.


Amesema kituo cha afya Mirerani kinahudumia wagonjwa wa kata za Endiamtu, Mirerani, Naisinyai na Shambarai Wilayani Simanjiro, Makiba, Mbuguni na Majengo Wilayani Arumeru Mkoani Arusha na Kata ya Mtakuja Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.


"Dawa zikiletwa leo zinakaa siku tatu zinaisha kutokana na idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa kwani hii ni huduma ya Serikali huwezi kukataza watu kutoka mikoa mingine wasipate huduma hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipopita kwenye kampeni aliahidi kuwa kituo hiki kinapandishwa hadhi kuwa hospitali tunaomba kiongozi wetu uliangalie hili kwa jicho la pekee na la huruma wananchi wanateseka mno kwenye hili," amesema Diwani Luka.


Akizungumzia suala la maji Diwani Luka amesema kuna tatizo la maji, watu ni wengi maji hakuna, kwenye shule hakuna maji, ambapo maji ndiyo kila kitu kwenye jamii, hivyo amemuomba Katibu Mkuu kuhakikisha analichukua hilo.


"Pamoja na hayo tunaomba mji mdogo wa Mirerani kuwa mji kamili Ili kusogeza karibu huduma kwa jamii kwani kufika makao makuu ya halmashauri inakulazimu usafiri kilomita 122," amesema.


Akijibu maombi hayo Chongolo amesema suala la kituo cha afya Mirerani kuwa hospitali anamuagiza Waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki atimize hilo kwani hospitali ya Wilaya ya Simanjiro ipo Orkesumet zaidi ya kilomita 122 hivyo Mirerani inapaswa kuwa na hospitali yake 


"Hili ni dogo kwangu silipeleki kwa Rais Samia Suluhu Hassan nitashughuhulikia mwenyewe andaeni eneo la kujenga hospitali," amesema Chongolo.


Kwa upande wa maji Chongolo amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kusambaza maji maeneo ya pembezoni hivyo wakazi wa mji mdogo wa Mirerani wasihofu juu ya hilo.


Hata hivyo, kwenye suala la mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani kuwa mji kamili, Chongolo amesema hilo litakuwa gumu kwa sasa kwani bajeti ya kuanzisha mji kutoka mji mdogo ni kubwa.


"Kuendesha mji mpya inabidi kuwa na shilingi bilioni 15 kwa mwaka isitoshe kuna maombi ya majimbo mapya 67 nchini hivyo suala la Mirerani kuwa mji kamili tuliache kwanza," amesema Chongolo.


Hata hivyo,  mkazi wa Kata ya Endiamtu, Sokota Mbuya amepongeza kitendo cha Diwani Luka kuwasilisha changamoto zinazowakabili wananchi kwa wakati sahihi pindi alipopatiwa nafasi.


"Unapokuwa mwakilishi wa wananchi unapaswa kufanya mambo ya namna hiyo kwani Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara mama Naomi Kapambala alipompa nafasi Diwani wetu naye akatiririka kwa hoja zake maridhawa ambazo ni changamoto zinazotukabili," amesema Sokota.


No comments: