DKT. BITEKO ATAKA WATUMISHI MADINI KUFIKIA MALENGO MAKUBWA YA SERIKALI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 11 March 2023

DKT. BITEKO ATAKA WATUMISHI MADINI KUFIKIA MALENGO MAKUBWA YA SERIKALI

 

Waziri wa Madini Dkt. Biteko





- Katibu Mkuu Mahimbali ataka  Wataalam  Sekta ya Madini kuweka Msukumo katika Madini Kimkakati


- Naibu Katibu Mkuu Mbibo awakumbusha watumishi kutambua matarajio ya Watanzania Sekta ya Madini


Greyson Mwase na Asteria Muhozya – Dodoma

maipacarusha20@gmail.com

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Wizara inayo majukumu  makubwa iliyopewa na Serikali ikiwemo kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.


Ametaka kazi kuwa kipimo cha ukaribu cha utendaji wa kazi  kwa watumishi wa wizara na taasisi katika kufikia malengo hayo na kuongeza kwamba, Wizara itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi pamoja na taasisi zilizopo chini yake ili kukuza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.


Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Machi 10, 2023 kwenye kikao chake na watendaji wa Wizara na Tasisi zake kilichofanyika jijini Dodoma  wakati akimkaribisha na kumtambulisha Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo.


“Kama Wizara tutaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua na mchango wake kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa watumishi wetu pamoja na taasisi tunazozisimamia ili kutoa ari ya kuchapa kazi kwa ubunifu na hata kuvutia watumishi wengine kufanya kazi katika Sekta ya Madini,”amesema Waziri Biteko.


Katika hatua nyingine, amempongeza Katibu Mkuu mpya wa Wizara Mahimbali kwa uteuzi wake na kuongeza kuwa, Wizara na Taasisi zake itaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha lengo likiwa ni kuifanya Sekta ya Madini kuwa miongozi mwa sekta zinazochochea uchumi wa nchi.


Naye, Katibu Mkuu Mpya Wizara ya Madini Kheri Mahimbali akizungumza katika kikao chicho amewataka wataalam wa Wizara kuweka msukumo kwenye madini ya Kimkakati kutokana na umuhimu wa madini hayo katika kuyafungamanisha na sekta nyingine za kiuchumi.


Amepongeza uongozi na watendaji wa Wizara na taasisi zake kwa kuiwezesha sekta ya Madini kufikia asilimia 9.7 ya mchango wake katika Pato la Taifa na kuwataka kuhakikisha asilimia 0.3 iliyobaki inafikiwa na kuongeza, ‘’tumeletwa hapa kuongeza nguvu, sikuja kumwondoa yoyote kwenye nafasi yake, bado tuna kazi mbele yetu na ninaamini katika kushirikiana,’’.  


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewataka watumishi Wizara ya Madini kutambua dhamana kubwa waliyonayo na matarajio waliyonayo watanzania kupitia rasilimali madini na hivyo kuwataka watumishi kuhakikisha rasilimali madini zinachochea uchumi wa nchi, ukuaji wa sekta nyingine na maendeleo ya watu.


Awali, watendaji kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara wakiwasilisha taarifa za utekelezaji  wa majukumu yao  katika kikao hicho, sambamba na kupongeza uteuzi wa Mahimbali wameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini.


Akizungumzia mafanikio ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Kaimu Mtendaji Mkuu Notka Banteze amesema hadi sasa GST imefanikiwa kufanya tafiti za jiolojia kwa asilimia 97 nchi nzima, jeokemia asilimia 24  high density,  asilimia 84 low density na  geophysics asilimia 16.


Akizungumzia mafanikio ya Tume ya Madini tangu kuanza kwa utekelezaji wa majukumu yake mapema Aprili 2018, Katibu Mtendaji wake Mhandisi Yahya Samamba ameeleza kuwa Tume imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.54 ikiwa ni sawa ya asilimia 91.43 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.77, uanzishwaji wa masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi wa madini nchini 93.


 Aidha, Mhandisi Samamba ameongeza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa thamani ya madini yaliyouzwa nje ya nchi kutoka kilogramu 53,173.39 yenye thamani ya shilingi trilioni 3.547 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 hadi kilogramu 60,184.8 yenye thamani ya shilingi trilioni 7.336 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 na kupungua kwa ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.


Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Nsalu Nzowa ameeleza mafanikio ya shirika hilo kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kujiendesha kibiashara na kutoa gawio la hisa Serikalini, kupata zabuni mbalimbali za huduma ya uchorongaji migodini na kuendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji katikaRasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Miriam Mgaya ameongeza mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji katika mapato yatokanayo na rasilimali za mafuta, madini na gesi asilia na kusisitiza kuwa mpaka sasa TEITI imechapisha ripoti 12.


Naye, Kaimu Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Daniel Kidesheni ameishukuru Wizara kwa kukiwezesha kituo hicho kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi ambayo itakisaidia kituo hicho kupiga hatua kubwa katika sekta ndogo ya uongezaji thamani madini.


Pia, ameeleza kuhusu mipango kabambe ya Kituo hicho ambayo inalenga kukiwezesha kuwafikia watanzania  kwa kiasi kikubwa hatimaye kuongeza wigo katika shughuli za uongezaji thamani madini.

No comments: