ZIARA YA MBUNGE WA JIMBO LA KIBAHA VIJIJINI, MWAKAMO YAIBUA CHANGAMOTO KITUO CHA AFYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 4 March 2023

ZIARA YA MBUNGE WA JIMBO LA KIBAHA VIJIJINI, MWAKAMO YAIBUA CHANGAMOTO KITUO CHA AFYA

Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo alipotembelea kituo hicho na wodi za wazazi kujionea mazingira ya kujifungulia na vikwazo vilivyopo katika kituo hicho


Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo alipotembelea kituo hicho na wodi za wazazi kujionea mazingira ya kujifungulia na vikwazo vilivyopo katika kituo hicho

 


NA: JULIETH MKIRERI, MAIPAC KIBAHA 


maipacarusha20@gmail.com 


MRATIBU wa afya ya Uzazi na mtoto katika Kituo cha Afya Mlandizi Kibaha Happiness Ndelwa amesema kitendo cha baadhi ya wanaume kushindwa kushiriki kwenda kliniki na wake zao ni moja ya sababu ya kukwama kununua vifaa vinavyotakiwa wakati wa kujifungua.


Ndelwa alisema, baadhi ya Wanawake wanafika katika kituo hicho bila kuwa na vifaa wanavyotakiwa kuwa navyo wakati wa kujifungulia jambo ambalo linawafanya uongozi wa hospitali kufanya jitihada kuvipata.


Hayo yamebainishwa wakati Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo alipotembelea kituo hicho na wodi za wazazi kujionea mazingira ya kujifungulia na vikwazo vilivyopo katika kituo hicho


"Wapo baadhi ya wanaume hawataki kushiriki na wake zao kuja Hospitali wanaona kufanya hivyo ni kupiteza muda bila kujua kuwa huko ndiko wanaelezwa kila kitu anachotakiwa mama mjamzito kubeba anapokuja kujifungua" alisema Ndelwa.


Mratibu huyo alimuomba Mbunge huyo wanapokuwa kwenye mikutano kuzungumzia suala hilo ili kuwaondolea vikwazo wauguzi.


Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Yahaya Mbogolume alimueleza Mbunge huyo kuwa wapo wanawake wanaofika kujifungulia katika kituo hicho bila vifaa walivyoelekezwa kuchukua mbali ya vinavyotolewa na Serikali. 


Awali muuguzi kiongozi wodi ya Wazazi katika kituo hicho Exaveria Kapulula alisema kuna wakati wazazi wanalazimika kulala kitanda kimoja wawili baada ya kujifungua kutokana na ongezeko la wateja katika wodi hiyo.


Kapulula alisema uwezo wa kituo hicho katika wodi ya wazazi ni kuhudumia wanawake 77 kwa mwezi wanaofika kujifungua lakini wamekuwa wakihudumia 282 kwa muda huo. 


Mwakamo alisema Serikali inafahamu vikwazo kwenye huduma za afya na zinaendelea kutatuliwa ili wananchi wanufaike na kuondokana na msongamano uliopo kwenye baadhi ya vituo.

No comments: