KAFULILA AJA NA MKAKATI WA KUVUTIA SHILINGI TRILLION 21 ZA PPP - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 25 April 2023

KAFULILA AJA NA MKAKATI WA KUVUTIA SHILINGI TRILLION 21 ZA PPP




Mwandishi Wetu, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Serikali imepanga kukutanisha wakuu wa mashirika ya umma 7 ya kimkakati na wabobezi wa uwekezaji wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) mwezi ujao kwa lengo la kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuvutia mitaji ya kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 9 (sawa na Sh. trilioni 21) ndani ya miaka mitatu.


Kamishna wa PPP Wizara ya Fedha na Mipango, David Kafulila ameseema kuwa mkutano huo utakaofanyika Mei 2-6 ni sehemu ya mkakati wa kufikia malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDPIII).


Akizungumza katika mkutano kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na wahariri jijini Arusha leo, Kafulila alisema kuwa wabobezi hao wa PPP wanatarajiwa kutoka kwenye taasisi za Benki ya Dunia ya International Finance Corporation (IFC).


Kafulila alibainisha kuwa warsha hiyo ya wabobezi itafunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na kwamba kila taasisi husika za umma, ikiwemo TANESCO, REA, TRC, TAA, TPDC, DART na TPA zitabainisha namna zilivyojipanga kutekeleza miradi kwa utaratibu wa PPP ndani ya miaka mitatu.


"Serikali imejipanga kutumia fedha kununua utaalamu kuhakikisha miradi ya PPP inaandaliwa kwa weledi mkubwa kuvutia mitaji duniani," alisema.


Alisisitiza kuwa mpaka sasa kuna miradi minne ya PPP sokoni, na mingine 21 iko katika hatua ya upembuzi.


"Miradi ya PPP iliyopo sokoni kwa sasa ni pamoja na mradi wa Expressway Kibaha- Chalinze,  BRT, Ujenzi wa hoteli ya nyota 5 uwanja wa Julius Kambarage Nyerere International Airport (JNIA), pamoja na ujenzi wa Business Complex," alisema.


Kafulila alisisitiza kuwa PPP ni ajenda kubwa ya duniani sasa kwa sababu mahitaji ya wananchi ni makubwa kuliko uwezo wa Serikali kufikia kwa kutumia mikopo na kodi. 


Alisisitiza kuwa deni la Taifa kwa Tanzania la takriban asilimia 40% ya uchumi ni kiwango cha wastani na himilivu na kwamba kama nchi tunafanya vizuri kulinganisha na nchi zote afrika mashariki na nyingi kusini mwa afrika kwa mujibu wa ripoti zote za taasisi ya Moody's. 


Hata hivyo, aliongeza kuwa pamoja mwenendo mzuri wa usimamizi wa uchumi na deni,  tafiti zinaonesha kwamba tuendako mahitaji ya miundombinu yatakuwa makubwa sana na hivyo kuepuka kuumiza wananchi kwa kodi kubwa na mikopo zaidi, ni lazima kutazama PPP kama mbadala nafuu.


"Tafiti zinaonesha kuwa miundombinu tuliyonayo Tanzania sasa hivi ambayo tumejenga kwa takriban karne moja, mfano reli ya kati, inatosha theluthi moja tu ya mahitaji ya taifa ya miundombinu ifikapo mwaka 2050," aliongeza.


Hivyo kutoka sasa na 2050 tunahitaji kujenga miundombinu mara mbili ya iliyopo sasa, alisema.



No comments: