Mtafiti wa Wanyamapori Dk Benard Kisuwi akizungumza na wadau wa Uhifadhi |
Maafisa wa Taasisi ya Chemchem ambazo walidhamini kongamano Hilo wakimsikiliza kwa makini wasilisho la Dkt kisuwi |
Picha ya pamoja baada ya kongamano |
Na: Andrea Ngobole, Babati
maipacarusha20@gmail.com
maipacarusha20@gmail.com
Wadau wa Uhifadhi mkoa wa Manyara wameomba Wakala wa Barabara (TANROADS ) mkoa Manyara kuharakisha uwekaji vibao vya tahadhari juu ya uwepo wanyama wanaovuka barabara ya Manyara-Arusha katika eneo la Jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge ambapo kila siku Mnyama mmoja anagongwa.
Takwimu katika eneo hilo zinaeleza kwa mwaka wanyamapori 380 wamekuwa wakifa kwa kugongwa na magari katika eneo hilo ambalo lipo katikati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa Uhifadhi mkoa wa Manyara, Mtafiti wa Wanyamapori Dk Benard Kisuwi alisema katika eneo la Burunge WMA licha ya vifo vya wanyamapori kugongwa na magari pia kuna changamoto ya wanyama wakali.
Alisema kikao hicho kina lengo la kuendeleza mikakati ya kutatua migogoro baina ya Wanyamapori na binaadamu katika eneo hilo.
Afisa Wanayamapori mkoa wa Manyara, Felix Mwasenga alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori wameanza mikakati kudhibiti vifo hivyo kwa kuweka vibao vya tahadhari
Alisema mkakati uliopo Sasa ni kuongeza vibao vya barabarani vya tahadhari kuonesha uwepo wanyamapori katika eneo hilo na kuwataka madereva kuwa makini wanapofika katika eneo la Magugu hadi Minjingu ambapo ni Mapito ya wanyamapori.
Afisa Mhifadhi mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori(TAWA) Aliningo Swai alisema katika eneo hilo pia kuna changamoto ya ongezeko la shughuli za kibinaadamu katika eneo lililotengwa kwa uhifadhi.
Swai alisema licha ya kazi nzuri ambayo inafanywa na Burunge WMA,wahifadhi na taasisi ya Chemchem ambao wamewekeza katika eneo hilo bado kuna matukio ya ujangili ambao unapaswa kukomeshwa.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano kutoka Chem chem Association Charles Sylivesta alisema wanaiomba serikali kuongeza kuweka vikao vya tahadhari katika eneo hilo.
Alisema katika hifadhi hiyo licha ya changamoto za kugongwa wanyama na ujangili bado idadi ya Wanyamapori imeongezeka kutokana na kazi nzuri ya uhifadhi.
" Sensa ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitano huku lengo likiwa ni kubaini idadi ya wanyama katika eneo la ikolojia ya Tarangire na Manyara inaonekana wanyama kuongezeka"alisema
Sylivesta pia alisema Ili kupunguza migogoro ya binaadamu na wanyama taasisi Yao imekuwa ikiwajengea mazizi ya chuma wafugaji Ili kuzuia wanyama wakali hasa Simba kuingia katika makazi na kula mifugo nyakati za usiku.
Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise alisema hifadhi hiyo ambayo inaundwa na Vijiji 10 imekuwa ikikabiliwa na changamoto la ongezeko la shughuli za kibinaadamu hifadhini ikiwepo, kilimo,ufugaji na makazi
Hata hivyo amesema kwa kushirikiana na wadau wengine wa Uhifadhi na Serikali wamekuwa wakitoa elimu ya kukomeshwa uvamizi ikiwepo pia kupambana na ujangili na ukataji wa miti na uvuvi haramu.
No comments:
Post a Comment