KATA NNE KUNUFAIKA NA MRADI MPYA WA MAJI NACHINGWEA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 22 August 2023

KATA NNE KUNUFAIKA NA MRADI MPYA WA MAJI NACHINGWEA

  




Na Mwandishi wetu, Nachingwea



WAKAZI 19,110 wa vijiji 11, Kata nne, Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji Naipanga, kupitia mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijiji (RUWASA).


Mradi huo wa thamani ya Sh1.1 bilioni utakuwa na tenki moja la ujazo wa lita 300,000 na uzio, vituo 40 vya kuchotea maji vyenye sehemu mbili na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 32,425.


Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo akizungumza wakati akitambulisha mradi huo kwenye kata ya Naipanga amewataka wanufaika wa mradi huo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi.


Moyo amewataka wanufaika watakaopitiwa na mradi huo kutokwamisha au kupinga kwani hakuna fidia watakayolipwa kwenye maeneo yao.


"Msikubali mtu mmoja au wawili wasababishe watu 19,110 wakose maji kisa bomba limepita kwenye shamba la mbaazi au korosho hivyo asikwamishe mradi kwa vile anataka fidia," amesema Moyo.


Amemuagiza mkandarasi wa mradi huo kuwapa kipaumbele na kutoa ajira kwa vijana na wanawake wa eneo hilo la mradi utakaopitiwa ili wajiongezee kipato.


Meneja wa RUWASA wilaya ya Nachingwea, mhandisi Sultan Ndoliwa ametaja kata zitakazonufaisha na mradi huo ni Naipanga, Chiumbati, Raha Leo na Stesheni.


Ametaja vijiji vitakavyonufaika ni Chiumbati shuleni, Chiwindi, Tandika, Joshoni, Nagaga, Maendelea, Kilombero, Naipanga, Luagala, Raha Leo na Chekereni.


"Kazi zote za mradi zilizopangwa kufanyika za ujenzi wa tenki la maji ujazo wa lita 300,000 ujenzi wa vioski 35, ujenzi wa vilula vitano na uchimbaji mitaro na ulazaji bomba kilomita 32,425 zimekamilika," amesema mhandisi Ndoliwa.


Mhandisi Ndoliwa ametoa rai kwa wanufaika wa mradi huo kumpa ushirikiano wa kutosha mkandarasi ili aweze kufanikisha majukumu yake.


Mkandarasi wa mradi huo mkurugenzi wa kampuni ya Broadways Engineering LTD, Shaban Kimaro amesema wakazi wa eneo hilo wakimpa ushirikiano wa kutosha kazi itamalizika kwa wakati muafaka.


Mkazi wa kijiji cha Chiumbati, Nachumwa Ally ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huo kwani awali walikuwa wanafuata huduma hiyo umbali mrefu.


No comments: