WAZIRI MCHENGERWA AZITAKA BODI TANAPA NA TTB, KUONGEZA IDADI YA WATALII WAFIKIE MILIONI 3 KUTOKA CHINA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 22 August 2023

WAZIRI MCHENGERWA AZITAKA BODI TANAPA NA TTB, KUONGEZA IDADI YA WATALII WAFIKIE MILIONI 3 KUTOKA CHINA






Na Mwandishi Wetu, ARUSHA

 

maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Mali asili na Utalii Mohamed Mchengerwa amezindua bodi mbili za wakurugenzi wa Shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa) pamoja  na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),alizoziteua hivi karibuni na kuzitaka bodi hizo kuhakikisha zinapadisha kiwango cha watalii kuingia nchini.


Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa kituo cha mikutano cha kimataifa (Aicc) jijini Arusha,waziri Mchengerwa alimpongeza RAIS Samia Suluhu  kwa kumteua tena, Jenerali mstaafu George Waitara kuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini TANAPA pamoja na balozi dkt. Ramadhan Dau kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TTB.


Alisema  uteuzi huo umezingatia weledi ,uzoefu ,uchapa kazi na uzalendo katika kutumikia taifa na kuzitaka bodi hizo kusimamia maslahi mapana ya nchi katika kukuza uchumi wa taifa, upatikanaji wa fedha za kigeni na uzalishaji ajira.


Alizitaka bodi hizo kukidhi malengo ya taifa ya mwaka 2020/25 ya kuhakikisha idadi ya  watalii milioni 5 na mapato ya taifa ya dola za kimarekani bilioni 6  yanafikiwa.


"Ninaimani Taasisi ya Tanapa inayosimamia vivutio vyetu ya utalii ikiwemo hifadhi ya Serengeti na mlima Kilimanjaro pamoja na bodi ya Utalii yenye dhamana ya kutangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi, zitachochea kwa kiasi kikubwa kufikia malengo hayo"


Aliitaka bodi ya utalii Tanzania kujipanga kikamilifu ili kuongeza idadi ya watalii ukizingatia kwamba idadi ya watalii  wa sasa ni ndogo ukizingatia  ukubwa wa nchi, wingi wa hifadhi pamoja na vivutio vilivyopo haviendani na idadi hiyo ya watalii.


Aliitaka bodi hiyo ya utalii kufanyakazi usiku na mchana kujiboresha na kuondokana na utendaji wa mazoea ili kwenda na kasi ambayo rais Samia anaihitaji ya kutangaza vivutio na kuongeza idadi ya watalii nchini.


"Huko nyuma kupitia mitandao ya kijamii wadau wetu wa utalii wamekuwa wakilalamika sana kwamba viongozi wa bodi ya utalii wamekuwa wakisafiri kwa ajili ya kufanya shopping nje ya nchi wakati mwingine tulipata aibu nchini Korea kusini walitengeneza maboksi kutangaza utalii wa Tanzania hii ni aibu kubwa"


Akitolea mfano suala la  uwekezaji wa vyumba vya kulala wageni hapa nchini ,alisema kuna vyumba takribani 120,000 kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na nchi ya Kenya ambayo inavyumba zaidi ya milioni 1.5.


"Tuna kwenda kufanya mapitio ya sheria itakayowapa mamlaka ya kuhakikisha mnaishauri serikali kwenye eneo la uwekezaji na kujua ni namna gani tunakwenda kuongeza idadi ya watalii,kuongeza vyumba vya  kulala watalii na eneo la ukarimu"


Alisema mpango mwingine wa TTB ni kuhakikisha inateka soko la watalii wanaotoka China kwani hivi sasa ni watalii 34,000 tu wanaokuja nchini wakati watalii wanaotoka china kwenda mataifa mbalimbali duniani wanakaribia milioni 200 kwa mwaka, hivyo ni lazima walau watalii milioni 3 kutoka China waje hapa nchini.


Aidha alisema takwimu zinaonesha kwamba bado hatujalifikia soko la watalii  wengi duniani hasa kutoka bara la Asia.


Akiongea mara baada ya kuzinduliwa kwa bodi hizo ,Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TANAPA, Jenerali mstaafu George Waitara, alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumwamini na kumteua katika kipindi kingine cha tatu kuongoza bodi hiyo.


"Natambua rais Samia ametuamini na sisi kazi yetu ni kuchapa kazi hatutamwangusha na imani hii tutailinda tunachohitaji kwako ni ushirikiano tu "


Walitara alitoa onyo kwa majangili walioanza kujitokeza ambao aliwaita ni wadogozi kwani kazi kubwa ya kutokomeza ujangili nchini imefanyika hasa baada ya kuzinduliwa kwa jeshi Usu.

No comments: