NA MWANDISHI WETU, MAIPAC CHALINZE
UWEPO wa kliniki za ardhi katika Halmashauri ya Chalinze unakwenda kurahisishia wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda Bagamoyo na Kibaha kwa ajili ya kesi za migogoro ya ardhi.
Ofisa ardhi wa Halmashauri hiyo Deo Msilu amesema kwamba katika kliniki hiyo ambayo itakuwa inazunguka katika kata za Bwilingu, Vigwaza, Msata ambapo wananchi wa kata za hizo na za karibu watafika kupatiwa huduma.
Ameyasema hayo Mjini hapa muda mfupi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash kuzindua kliniki hiyo kwa Halamashauri hiyo.
Msilu amebainisha kuwa katika kliniki hiyo wananchi wenye malalamiko na migogoro ya ardhi watapata huduma kutoka kwa wanasheria na mawakili bure.
Kwa mujibu wa Msilu migogoro ya ardhi ambayo imeshamiri kwenye Halmashauri hiyo ni ya wakulima na wafugaji, mipaka kati ya kijiji kimoja na kingine na uvamizi wa maeneo ya Serikali, hifadhi na Mashamba yaliyotelekezwa.
" Kata zinazoongoza kwa migogoro ni pamoja na Ubena, Mbwewe, na Kiwangwa, maeneo yote hayo tumeshapita kutoa elimu na tunaendelea kufanya hivyo ili wajue sheria na kuziheshimu kwani kwa kufanya hivyo itapunguza muingiliano kwenye matumizi ya ardhi" amesema.
Salma Mrisho mmoja wa wakazi wa Chalinze alipongeza uamuzi wa Mkuu huyo wa Wilaya kuanzisha kliniki hiyo ambayo itawapa fursa ya kusikilizwa malalamiko yao sambamba na kupunguziwa gharama za kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma hiyo.
Katika siku ya kwanza ya uzinduzi wa kliniki hiyo Halmashauri ya Chalinze wananchi zaidi ya 30 walijitokeza kupata huduma.
Kliniki ya ardhi kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi lizinduliwa katika Wilaya ya Bagamoyo na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa na baadae Mkuu wa Wilaya hiyo Halkma Okash kufanya uzinduzi huo kwa Halmashauri ya Chalinze.
No comments:
Post a Comment