Dkt. Anna Henga Mkurugenzi mtendaji wa LHRC akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mapema leo |
Na: Andrea Ngobole, Arusha
Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) kimeitaka
serikali kuunda tume maalaum au kikosi kazi kitakachofanya kazi ya uhakiki wa
mipaka katika maeneo yote ya hifadhi ambayo yamekuwa yakisababisha migogoro
kati ya wananchi na mamlaka za hifadhi.
Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za Binadamu
nchini, Dkt Anna Henga amesema hayo jijini Arusha leo alipokuwa akisoma taarifa
ya hali inayoendelea Ngorongoro ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa
utekelezaji wa uhamishaji wa wakazi wa ngorongoro kweda Msomera.
Amesema wao kama watetezi wa haki za binadamu hawapingi
kuhamishwa kwa wakazi walioridhia kuhama isipokuwa zoezi la uhamishaji wakazi
hao lisitumike kuwanyanyasa wakazi ambao hawajaridhia kuhama.
Amesema ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaonekana Zaidi
katika huduma za elimu na afya ambapo watoto 24,000 hawajapata huduma yoyote ya chanjo
kama watoto wengine nchini, wanawake wajawazito 5,700 hawajapata huduma,
matibabu, chanjo na ushauri wa afya wakati wa ujauzito, wagonjwa 145 wenye TB
sugu hawajapata dawa na wagonjwa 84 wenye VVU hawajaweza kupata dawa za
kufubaza virusi vya ukimwi na hivyo kutishia uhai wao.
Amesema adha hiyo imetokana na serikali kusitisha huduma za kijamii
kwa kutoendeleza miradi na kusitisha huduma kwa kuondoa fedha katika taasisi
mbalimbali na kutopanga bajeti ya fedha 2022/23 na 2023/24 kama kuondolewa kwa
fedha za vifaa tiba milioni 500 za zahanati ya Nainokanoka kupelekwa Msomera, million
80 za ujenzi wa kitengo cha wagonjwa wa nje zahanati ya Osinoni kuondolewa na
fedha za zahanati nyingine zimeondolewa tangu mwezi April 2022.
Ameendelea kusema kuwa serikali imeondoa shilingi milioni 500
kwa hospitali ya Endulen kama ruzuku toka mwaka 2020, na kuathiri wananchi
100,000 wa tarafa ya Ngorongoro wanaoitegemea hospitali hiyo.
Ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu ulioanishwa katika
taarifa hiyo ni huduma za Elimu ambapo Jumla ya shilingi million 256 za shule
za msingi za Irkipori, Endulen na Ereko na kuhamishiwa shule misngi Msomera, milioni 790 za ujenzi wa bweni, shule mpya ya
Endulen na madarasa mapya nazo zimeondolewa.
Taarifa hiyo Imesema kuwa jumla ya shilingi milioni 720 za ujenzi wa madarasa,
mabweni na mabwalo katika shule za sekondari za Ngorongoro Girls, Embarway na
Nainokanoka zimeondolewa na kusitisha mpango wa ujenzi katika shule hizo.
Huduma za ujenzi wa miradi ya maji katika kata za Ngoile million
200, kata ya Masamburai million 151, kata ya Olbalbal milioni 200 na kata ya
Alaililai million 146 zimeondolewa na kusababisha adha kwa wananchi waliopo
katika kata hizo.
Amesema kuwa kwa takribani mwezi sasa wananchi 48
wamekamatwa, kushikiliwa Zaidi ya muda unaoruhusiwa kisheria bila kupewa haki
ya kuwasiliana na familia wala wanasheria wao, viongozi wa ngazi zote kata ya
Endulen wamekamatwa kwa madai ya kuhasisha wananchi wao kudai huduma za
kijamii.
Amesema kituo hicho kinatoa wito kwa serikali kuwa mchakato
unaoendelea wa kuhamisha wananchi usitumike kuwanyanyasa, kuwanyima huduma za
kibinadamu, kuwashurutisha kuondoka pasi na ridhaa yao.
Kuzingatia haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa amri za
kuwaondoa na kuwahamisha wananchi katika hifadhi, serikali isimamie ahadi yake
kuwa wananchi wanaohamishwa Ngorongoro ni wale waliokubali wenyewe kuhama na
wale wasiotaka kuhama waachwe na wapewe huduma za kibinadamu kama watanzania
wengine.
Amesisitiza kuwa tume ya haki jinai hasa jeshi la Polisi na
majeshi usu iweze kufanyiwa kazi mapema ili kuimarisha ulinzi wa haki za
binadamu.
No comments:
Post a Comment