Majambazi yapora 30 milioni ,Walinzi waliofungua Mlango watoweka. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 14 September 2023

Majambazi yapora 30 milioni ,Walinzi waliofungua Mlango watoweka.

 


Mlinzi aliyekuwepo siku ya tukio na kutoroka 

Mlinzi aliyekuwepo siku ya tukio na kutoroka


Mwandishi wetu, Arusha


maipacarusha20@gmail.com



Watu saba wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakiwa na silaha wamevamia nyumbani kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Predators Safari Club na Arusha Water Drilling,Yusuph Khan  na kupora fedha taslimu shilingi milioni 30 na vidani vya dhahabu vyenye thamani ya sh 15 milioni.


Tukio hilo, limetokea Septemba 10, saa 2 usiku katika eneo la Kiranyi Sakina, wilayani Arumeru, baada ya majambazi hayo, kumvamia Mkurugenzi huyo, wakati akiingia nyumbani kwake.


Kutokana na Tukio hilo, Jeshi la polisi mkoa Arusha limeanza  uchunguzi wa tukio hilo na  msako wa kuwasaka waliohusika.


Hata hivyo, Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi Bado unaendelea.


Khan amesema majambazi hayo, kabla ya kufanya uporaji huo, yalifunguliwa lango la kuingia ndani na walinzi wa kampuni binafsi  Mwengwe ambao nao baada ya tukio hilo walikimbia na majambazi hao.


"Nilikuwa na familia yangu naingia ndani na ndipo nilivamiwa na majambazi haya ambayo yalikuwa na silaha mbali mbali na kunijeruhi kisha kuingia ndani na kuchukuwa fedha na vito vya thamani baada ya kuwaweka chini ya ulinzi familia yangu "alisema


Alisema baada ya tukio hilo, walinzi waliokuwa zamu,Moses Alfred Mabula (46) na Lazaro Richard Pruza(37) wote wakazi wa eneo la Daraja mbili jijini Arusha walikimbia na kuondoka na majambazi hao.


"Kamera za usalama zinaonesha walinzi ndio waliwafungulia mlango majambazi na kuingia ndani kupora na baada ya hapo wamekimbia na hawajulikani walipo"alisema


Khan aliomba Jeshi la Polisi na Serikali kusaidia kukamatwa walinzi na majambazi hao, kwani fedha zilizoporwa alikuwa amepokea jumamosi jioni baada ya kuuza gari ya Mitsubishi Canter yenye namba za usajili T196 DRX .


"Baada ya tukio tulitoa taarifa polisi ambao walifika na kuanza uchunguzi na tayari kesi imefunguliwa"alisema


Meneja wa kampuni ya Predators Safaris  Club Ltd , Steve laizer alisema kampuni hiyo, itatoa zawadi ya shilingi 2 milioni mbili kwa ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na walinzi.


"Hili ni tukio la kupangwa sasa ambao atawezesha kukamatwa na polisi walinzi waliotoweka tutatoa zawadi ya sh  milioni mbili"alisema


Julius Manase mkazi wa Kiranyi alisema, walipata taarifa ya tukio hilo baada ya kuona kikundi cha watu wakikimbia usiku kutoka katika nyumba hiyo ambapo pia kuna Karakana ya magari.


"Huu ni wizi wa kupanga tunaimani watuhumiwa watapatikana kwani Arusha, tulianza kusahau matukio ya aina hii lakini sasa yameanza kurudi"alisema.

Meneja wa kampuni ya ulinzi ya Mengwe ,Juma Masuka alithibitisha kuwa walinzi hao wanatoka kampuni yake na sasa wanashirikiana na jeshi la polisi kuwasaka popote walipo na alitoa wito kwa wananchi kusaidia kukamatwa kwa walinzi wake wanaohusishwa na ujambazi

No comments: