UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA UNAVYOATHIRI WANAWAKE NA WATOTO WA KATA YA OLMOLOG WILAYANI LONGIDO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 14 September 2023

UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA UNAVYOATHIRI WANAWAKE NA WATOTO WA KATA YA OLMOLOG WILAYANI LONGIDO




Baadhi ya akina Mama wa kata ya Olmolg wilayani Longido wakiwa na ndoo tupu za maji

NA: ANDREA NGOBOLE, Longido


maipacarusha20@gmail.com

Upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya wanadamu ni moja ya huduma muhimu na ya lazima kwa maisha, ustawi wa wanadamu na maendeleo ya uchumi wa jamii.

Kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania serikali inawajibu wa moja kwa moja kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji safi na salama ili kulinda afya na uhai wa wananchi.


Wataalamu wa afya na mazingira wanabainisha kuwa utumiaji wa maji yasiyo safi na salama husababisha magonjwa ya mlipuko kama kuhara na kipindupindu ambayo husababisha vifo kwa wanadamu.

Popote penye ukosefu wa maji safi na salama mara nyingi waathirika wakubwa huwa ni akina Mama na watoto wenye jukumu la kusaka huduma hiyo kwa matumizi ya familia.

Adha hii ya ukosefu wa maji safi na salama inawakumba wakazi 8,764 wa vijiji vya Elerai, Lerangwe na Olmolog vinavyounda kata ya Olmolog wilayani Longido mkoani Arusha ambao wanakosa huduma ya maji safi na salama hali inayowalazimu kutembea umbali wa kilomita 10 kupata maji safi na salama kijiji cha Muton Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro.

Makundi ya wakina mama na watoto ndiyo wameathirika Zaidi na ukosefu wa maji safi na salama kwa kuugua magonjwa ya kuhara.

Sababu kuu inayopelekea adha hii kwa wakazi hao ni kutokamilika kwa mradi wa ujenzi wa Tenki la maji safi na salama ulioanza kujengwa mwaka 2021 na kupaswa kukamilika Juni 2022. Mradi wa tenki hili la maji na usambazaji wa maji ulitarajiwa kugharimu shilingi milioni 900 lakini mpaka sasa septemba 10, 2023 bado haujakamilika.

Mary Mollel (32) mkazi wa kijiji cha Olmolog anasema kuwa changamoto ya kusaka maji safi na salama inauwaumiza sana kwani inawalazimu kuamka usiku wa saa tisa kwenda kusaka maji na huenda kwa makundi ya akina Mama ili kukabiliana na hatari mbalimbali za wanyama wakali kama fisi na tembo na pia kuepuka kufanyiwa vitendo viovu vya ubakaji toka kwa wanaume wakware.

Anasema uzalishaji mali unapungua kwani wanatumia muda mrefu zaidi kwenda kusaka maji ambapo kama ujenzi wa mradi wa tenki la maji safi na salama ukikamilika utawasaidia sana katika kufanya shughuli zamaendeleo.


“Tunalazimika kwenda kijiji cha Muton wilaya ya Siha kusaka maji haya safi na salama kwa matumizi ya nyumbani ili kuwalinda watoto wetu na madhara ya kutumia maji yasiyo salama kwani madhara yake kiafya ni makubwa mie binafsi watoto wangu wawili walishaumwa na matumbo kwa kutumia maji yasiyo salama” Alisema Mary


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Lerangwe Stephano Laizer anasema pamoja na kwamba wamewaelimisha wananchi wao wavune maji ya mvua na kuhifadhi katika matenki yao lakini maji hayo hayatoshelezi mahitaji ya kaya hivyo kipindi hiki cha ukame wakazi hao wanalazimika kutumia kwa muda mrefu kwenda kuchota maji safi na salama na kathiri shughuli za uzalishaji katika familia.


Diwani wa Kata ya Olmolog, Loomoni Olesiato Mollel anasema watoto na akina Mama wa kata hiyo wanaathirika sana na ukosefu wa maji safi na salama kwani wamama wanatumia muda mrefu kusaka maji na kuathiri ndoa zao na uzalishaji wa mali na pia watoto kutoweza kuhudhiria masomo kwa wakati.


Kwa mujibu wa takwimu toka shirika la afya duniani (WHO) inasema Kila siku wanakufa watoto elfu sita ulimwenguni kutokana na maradhi yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Japokuwa maji ni muhimu kwa uhai wa viumbe, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hakuna uwiano wa mgawanyo wa maji ulio sawa kati ya sehemu moja na nyingine na katika majira mbalimbali ya mwaka. Aidha, wingi wa maji yanayofaa kwa matumizi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi una kikomo, na maji hayo pia yanaweza kuathirika kirahisi.

Aidha watu bilioni moja nukta moja wanakosa maji safi ya kunywa na wengine bilioni mbili nukta sita hawana njia ya kujipatia hata maji ya kujisafisha.

Sababu kuu inayoainishwa katika ripoti ya pili ya shirika la Umoja wa mataifa la kuhifadhi matumizi ya maji ulimwenguni ni utawala mbaya, rushwa na ukosefu wa vitega uchumi.

Serikali ya Tanzania katika sera ya maji safi salama inaainisha mkakati unaoelekeza kufikia mwaka 2025 maji yapatikane kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.

Kutokamilika kwaa mradi wa Tanki la maji safi na salama kata ya Olmolog kunawaathiri sana watoto na akina Mama, Halmsahauri ya wilaya ya Longido na Ruwasa hawana Budi kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili kuwaokoa wakazi hao na adha kubwa ya upatikanaji wa maaji safi na salama.

No comments: