SERIKALI NA CCM NZEGA ZAPONGEZWA NA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KWA USHIRIKIANO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 22 September 2023

SERIKALI NA CCM NZEGA ZAPONGEZWA NA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KWA USHIRIKIANO

 




Na Mwandishi wetu, Nzega


Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu wa 2023 Abdalla Shaibu Kaim ameipongeza Serikali ya Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, inayoongozwa na DC wake Naitapwaki Tukai kwa namna inavyoshirikiana vyema na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Kaim akizungumza baada ya mbio za mwenge wa uhuru kumaliza kukimbizwa kwenye Wilaya ya Nzega, amesema amekoshwa kwa namna ambavyo viongozi wa Serikali na CCM wanavyoshirikiana bega kwa bega katika kuijenga Nzega.


"DC Nzega mtu bingwa kabisa wa vitendo, unastahili pongezi kwa namna ambavyo mnashirikiana na chama tawala cha CCM katika uongozi wa Wilaya ya Nzega na mtafika mbali," amesema Kaim.


Amesema kwa muda wa siku mbili mwenge wa uhuru ulivyokuwa kwenye Halmashauri mbili za Wilaya ya Nzega na Mji wa Nzega ameuona ushirikiano mkubwa baina ya Serikali ya Wilaya na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


"Endelelezeni umoja, mshikamano na upendo uliopo kwa viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Nzega na CCM kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Nzega," amesema Kaim.


Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai amemshukuru kiongozi huyo wa mbio za mwenge kwa pongezi hizo kutokana na wao kushirikiana na CCM.


"Viongozi wa CCM ndiyo waajiri wetu hivyo, tunawaheshimu na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wakutosha na tunakuahidi kuwa tutaendeleza ushirikiano huu uliouona," amesema DC Tukai.


Amesema CCM ndicho chama kilichomlea hadi kusababisha yeye akateuliwa kuwa DC hivyo anatoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na chama hicho tawala katika kuwatumikia wana nzengo wa Nzega.


Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa kutoka Mkoa wa Manyara, Emmanuel Jackson Hondi, amewapongeza viongozi na wananchi wa  Wilaya ya Nzega kwa namna walivyokaa nao kwa muda wa siku mbili.


"Tunawakaribisha Mkoani Manyara Oktoba 14 kwenye kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ambapo Manyara itawaka moto kwenye Oktoba ya kibabe, kwaherini Nzega hodi Igunga," amesema Hondi. 



No comments: