Wizara Ya Maliasili Yaendelea Kukabiliana Na Changamoto Za Wanyamapori Waharibifu - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 24 September 2023

Wizara Ya Maliasili Yaendelea Kukabiliana Na Changamoto Za Wanyamapori Waharibifu

 






Na Valentine Oforo, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


WIZARA ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeingia makubaliano na Shirika la Chakula Duniani FAO (Ofisi ya Tanzania) kutekeleza programu maalumu ya kutoa elimu kwa umma juu ya namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori waharibifu.

Pamoja na mambo mengine, hatua hiyo imekuja kutokana na kuwepo kwa matukio mengi ya migogoro kati ya wanyamapori waharibifu na wananchi wanaoishi karibu na shoroba za wanyamapori hao nchini.

Katika hatua ya awali ya kuteleleza programu hiyo, wataalamu wa Wizara wamekutana na wenzao kutoka FAO mkoani Morogoro katika kikao maalumu cha kuandaa machapisho yatakayotumika kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na uharibifu unayofanywa na wanyamapori wakali na waharibifu.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Mafunzo na Takwimu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi amesema nia ya serikali ni kuona wanyamapori wanahifadhiwa vyema ili kupunguza migongano kati yao na binadamu.

“ Malengo haya yatawezekana kama kutakuwepo ushirikiano mzuri kati ya serikali na wananchi, hasa wale wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi, pamoja na shoroba za wanyamapori," amesema.

Akifafanua kwa kina, Dkt Kohi alisema lengo la kuandaa programu ya utoaji wa mafunzo hayo ni kuhakikisha wanyamapori wanastawi na kuhifadhiwa vyema, lakini pia, jamii zinazoishi karibu na wanyamapori hao zinastawi bila shughuli zao za kiuchumi kuathiriwa na wanyamapori," alisisitiza. 

"Kwa mfano, kumekuwa na matukio mabaya ambapo wananchi waishio karibu na shoroba za wanyamapori wamekuwa wakiuwawa vibaya na wanyamapori hao, hususan Tembo huku mazao yakiwa yanaharibiwa pia," aliongeza.

Ameongeza kuwa, kwa sasa wizara inatekeleza programu maalumu ya kukuza shughuli za utalii hapa nchini, sekta ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea kuwepo kwa ustawi mzuri wa wanyamapori," ameongeza.

Kwa upande wake, Mshauri wa Kitaifa  wa Kusaidia usimamizi wa migogoro kati ya wanyamapori na binadamu kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO), Bi.  Beatha Fabian amesema programu hiyo imelenga kusaidia na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori hao. 

“Najua kwa nchi yetu tuna hifadhi nyingi sana pamoja na maeneo mengine ya namna hiyo. Na migongano ya wanyama na binadamu haiepukiki. Hivyo Programu hii itasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto hizi za migongano baina ya binadamu na wanyamapori ” amesema Beatha.

Kikao hicho kinachofanyika mkoani Morogoro kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo TAWA, TAWIRI na TANAPA, wengine ni TNRF, Halmashauri ya Same, Mkinga, Lushoto, Korogwe   pamoja na wadau kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO).

No comments: