BILIONEA LAIZER AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 23 October 2023

BILIONEA LAIZER AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO

 




Na Mwandishi wetu, Simanjiro


maipacarusha20@gmail.com


MCHIMBAJI maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Kurian Laizer, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyotenga fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo hasa elimu.


Akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule ya msingi Naisinyai wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Bilionea Laizer amesema Serikali ya Rais Samia imefanya kazi kubwa. 


Katika mahafali hayo ambayo Bilionea Laizer alikuwa mgeni rasmi, pia kuliendeshwa harambee ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo na kupatikana fedha kiasi cha shilingi milioni 38.6.


Amesema kwenye kata ya Naisinyai kuna mradi mkubwa wa shule ya kidato cha tano na cha sita, ambapo Serikali ya Rais Samia imetoa fedha nyingi karibu shilingi bilioni moja.


“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imetenga fedha nyingi kwenye miradi ya elimu hivyo wafugaji tunapaswa kulipa hayo kwa kupeleka watoto wetu shule,” amesema Bilionea Laizer.


“Tuache watoto wetu wasome kwani hata kama sisi wazazi wao hatukupata elimu kubwa tuwajali watoto wetu kwa kuwasomesha wote bila kubagua wasichana,” amesema bilionea Laizer.


Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni amesema kiasi hicho cha fedha kilichopatikana kwenye harambee hiyo ya ujenzi wa uzio wa shule na kupatikana shilingi milioni 38.6 ni kizuri kwa kuanzia ujenzi.


Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Toima Mtero amemshukuru mgeni rasmi wa mahafali haya Bilionea Laizer kwa kutoa motisha ya shilingi milioni 1 kwa mwalimu mkuu na mpishi wa shule Sh500,000 ya zawadi.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Naisinyai, Agnes Chang’endo amesema imeanzishwa mwaka 1974 ikiwa na miaka 49 hadi hivi sasa ina wanafunzi 622.


Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni amesema ameitaka jamii ya eneo hilo kuona wasichana waliohitimu darasa la saba kama nyara ya serikali hivyo wasiwaoe waachwe wasome.  



No comments: