Tume ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu yashauri Matumizi ya Maarifa ya asili kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 28 October 2023

Tume ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu yashauri Matumizi ya Maarifa ya asili kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi

 



Mwandishi wetu.Arusha

maipacarusha20@gmail.com



Maarifa ya Jamii za asili katika uhifadhi wa mazingira yametakiwa kuanza kutumika barani Afrika ili kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi.


Maarifa hayo pamoja na maarifa ya kisasa yakitumiwa vizuri  yanaweza kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika.


Tume ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu (ACHPR) imeshauri kutumika maarifa ya asili kama ilivyo kwa maarifa mengine katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika.


Hayo yameelezwa  katika kikao Cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu (ACHPR) kinachoendelea Arusha, wakati wa mjadala kujadili rasimu ya ripoti ya athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa Haki za Binaadamu barani Afrika.


Kamishna wa Tume hiyo ,Solomon Dersso alisema suala la athari  za mabadiliko ya Tabianchi linagusa haki za Binaadamu hivyo ni muhimu kutumia pia maarifa ya asili na mengine kukabiliana nayo.


Alisema mabadiliko ya Tabia nchi yanaendelea kusababisha ukame, upungufu wa chakula na athari nyingine za jamii.


Amesema Jamii za asili barani Afrika zina maarifa na Mila ambazo zinaweza kutumika pamoja na Teknolojia za kisasa kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.


Wawakilishi wa Asasi za kiraia barani Afrika wameshauri badala ya serikali za Afrika kuendelea kuziona Jamii za asili kama ni waharibifu wa mazingira zinapaswa kutambua maarifa yao ya utunzwaji wa mazingira.


Jamii za asili barani Afrika zimetajwa kuwa ndio zimetunza ardhi yao, mazingira na vyanzo vya maji, ardhi ambayo imekuwa ikivutia uwekezaji na Uanzishwaji wa hifadhi za misitu na Wanyamapori.


Mwanaharakati Ayoo Julius Ojore wa Uganda ambaye anatoka Taasisi ya kusaidia Jamii za pembezoni Uganda alisema Jamii za pembezoni ama za asili zinamaarifa mengi ya uhifadhi wa mazingira ndio sababu Maeneo Yao yanakimbiliwa kuchukuliwa na serikali na wawekezaji


Alisema Jamii ya Batwa ambayo inapatikana milima ya Rwezori ka Betwet eneo la milima ya kween ni mfano wa Jamii ambazo zimetunza ardhi yao lakini badala ya kuendelezwa zimekuwa zikipata Shida na kuondolewa Kwenye ardhi.


Mkurugenzi wa Shirika la CILAO,  Charles Odero alieleza Tume hiyo jinsi walivyobaini Jamii za asili kuwa na maarifa mengi ya utunzwaji mazingira, vyanzo vya Maji na misitu kupitia mradi waliokuwa wakifanya na Shirika la kusaidia Jamii za pembezoni la MAlPAC.


Alisema katika mradi huo ambao ulikuwa unadhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia program ya miradi midogo iliyochini ya Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) wamebaini Jamii za asili zinamaarifa ambayo yanapaswa kuendelezwa.


Odero alisema mradi huo ambao wametekeleza katika wilaya tatu za Ngorongoro, Monduli na Longido umebainisha utajiri wa maarifa ya asili katika uhifadhi wa mazingira, misitu na Vyanzo vya maji lakini changamoto bado watungaji wa sera hawajaupa uzito.


Queen Bisseng wa  nchini Cameroon wa Shirika la kusaidia Jamii zilizotengwa Upande wa Afrika(GFOD) alisema ni muhimu Sasa Jamii za asili kunufaika na Rasilimali zake .


Bisseng alisema nchi nyingi Afrika bado hazijatambua umuhimu wa maarifa ya Jamii za asili hasa katika masuala ya uhifadhi mazingira, elimu, Afya ili kuweza kuendelezwa.


Mabadiliko ya Tabianchi yamekuwa na athari kubwa katika nchi nyingi kadhaa Duniani na hivyo kuanza kutajwa kama ni athari kwa Haki za Binaadamu.








No comments: