Baadhi ya akina Mama wa kata ya Olmolg wilayani Longido wakiwa na ndoo tupu za maji |
NA: ANDREA NGOBOLE, LONGIDO
Maipacarusha20@gmail.com
Ripoti mbalimbali za kila mwaka za wizara ya maji zinaonesha kwamba idadi ya watu wanaopata maji safi na salama katika maeneo ya vijijini ni ya kiwango cha chini ikilinganishwa na ile ya wanaoishi mjini, hata hivyo hali halisi inaweza kuwa mbaya Zaidi kulingana na jiografia ya eneo husika na miundombinu hafifu ya kufikisha maji katika maeneo ya vijijini.
Uhaba mkubwa wa miundombinu ya maji, matatiazo ya utunzaji wa miundombinu na kiwango kidogo cha ufahamu wa wakazi wa vijijini juu ya utumiaji wa maji safi na salama pia yanachangia hali kuwa mbaya zaidi kwa jamii za vijijini.
Dira ya 2025 ya serikali ya Tanzania inalenga kufikisha kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 90 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 100 kwa maeneo ya mijini kulingana na idadi ya watu ifikapo mwaka 2025.
Vijiji vya Elerai, Lerangwe na Olmolog vinavyounda kata ya Olmolog wilayani Longido mkoani Arusha vinakosa huduma ya maji safi na salama hali inayowalazimu wakazi wa vijiji hivyo kutembea umbali wa kilomita 10 kupata maji safi na salama kijiji cha Muton Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro.
Umbali huu wa kutembelea kilomita 10 kusaka maji unaathiri uchumi wa wakazi hao kwani hutumia muda mrefu kusaka maji badala ya kufanya shughuli zingine za uzalishaji mali kama anavyosema Naishiye Mollel mkazi wa kijiji cha Elerai.
’’Kwa kweli uzalishaji mali unapungua kwani tunatumia muda mrefu kutafuta maji badala ya kufanya shughuli zingine za maendeleo.’’ Alisema Naishiye
Mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi (MKUKUTA) unaozingatia kuongezeka kwa kiwango cha upatikananji wa maji kama moja ya kipaumbele katika ajenda yake aidha mpango wa maendeleo wa sekta ya maji unatekelezwa kwa kuzingatia sera ya taifa ya maji na mkakakti wa Taifa wa maendeleo ya sekta ya maji.
Hata hivyo ujenzi wa Tenki la maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu unaosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Longido Mkoani Arusha toka chanzo cha maji ya mto Simba na kisha kusambazwa kwa wakazi wa vijiji vinavyounda kata ya Olmolog Wilayani Longido ulioanza kujengwa mwaka 2021 na kupaswa kukamilika Juni 2022 mpaka sasa haujakamilika na kusababisha adha kubwa kwa wakazi hao.
Meneja RUWASA Wilaya ya Longido, Petro Nyerere, alisema mradi huo umechelewa kukamilika kwa sababu ya ukosefu wa fedha ya kumlipa mkandarasi takribani million 900 ila kwa sasa pesa zimepatikana na kutolewa kwa mkanadarasi hivyo watahakikisha mradi unakamilika ndani ya Miezi sita toka sasa.
Diwani wa Kata ya Olmolog, Loomoni Olesiato Mollel anasema kukosekana kwa maji safi na salama kumepelekea kuyumba kwa uchumi kwa wakazi wake kwani wanatumia muda mrefu kusaka maji badala ya kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali ambapo kama mradi wa ujenzi wa Tenki la maji safi na salama ukikamilika utasaidia sana kuinua uchumi wa wakazi hao
Kama inavyotambulika maji ni muhimu kwa uhai wa viumbe, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kukosekana kwa maji safi na salama kunakopelekea magonjwa ya mlipuko pia kunaathiri uchumi wa wakazi hao wanaofikia 8,764 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Elerai Simon Ole Nassari anasema katika kijiji hicho hawajawahi kupata huduma ya maji safi na salama hali inayopelekea kuathiri uchumi wa wakazi wake wanaotumia muda mrefu kusaka maji badala ya kujitafutia kipato.
‘’Kijiji chetu hakijawahi kuwa na maji safi na salama, wakina mama wanalazimika kwenda kusaka maji katika kijiji cha Muton wilaya ya siha na kutoka hapa hadi huko ni umbali wa kilomita 15, wakinamama hutumia muda mrefu kusaka maji hayo badala ya kufanya shughuli za uzalishaji mali’’. Alisema
Amesema changamoto kubwa ni akina mama hao kutumia muda mwingi sana kusaka maji ya matumizi ya nyumbani na hivyo kupunguza uzalishaji na hivyo kuzorotesha uchumi wa kaya hizo.
Upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya wanadamu ni moja ya huduma ya lazima kwa maisha na ustawi wa wanadamu. Kwasababu hiyo serikali inawajibika kwa mujibu wa Katiba kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji safi na salama ili kulinda afya na uhai wa wananchi
Serikali ya Tanzania katika sera ya maji safi salama inaainisha mkakati unaoelekeza kufikia 2025 maji yapatikane kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
Kutokamilika kwa mradi wa ujenzi wa Tenki la maji safi na salama kata ya Olmolog kunaathiri sana uchumi wa wakazi wa kata hiyo, Halmsahauri ya wilaya ya Longido na Ruwasa hawana Budi kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili kuwaokoa wakazi hao na adha kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment