Mwandishi wetu, Babati
maipacarusha20@gmail.com
Mahakama ya Hakimu Mkazi mfawidhi wa wilaya ya Babati mkoa Manyara, imemuhukumu kwenda jela miaka 23 , Amos Benard Mtinange maarufu kwa jina la Meja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ujangili wa Twiga na kuuza nyama za Twiga kinyume cha sheria
Meja alikamatwa April 21 mwaka 2022, saa kumi na moja jioni maeneo ya mfulwang'ombe kwenye Kambi ya samaki Kijiji cha Vilima vitatu, ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge wilayani Babati, mkoa wa Manyara baada ya kusakwa muda mrefu kutokana na kujihusisha na ujangili wa Twiga na kufanya biashara ya nyama za Twiga.
Alikamatwa kutokana na mtego ulioandaliwa na askari wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), Jeshi la polisi, Askari wa Burunge WMA na askari wa Taasisi ya Chem chem association ambayo imewekeza shughuli za Utalii katika eneo hilo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati, mkoa wa Manyara, Victor Kimario alisema, mahakama imemtia hatiani Meja baada ya kujiridhisha pasi na shaka kuwa amekuwa akijihusisha na ujangili wa Twiga na kuuza nyama za Twiga.
Alisema ili kukomesha matukio ya ujangili nchini, Mahakama inamuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 23 jela.
Kabla ya hukumu hiyo, Meja aliomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani anafamilia ambayo inamtegemea.
Hata hivyo, Waendesha Mashitaka wa Serikali Benedict Mapunda,na Mawakili wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori(TAWA) Getrude Kariongi na Shahidu Kajwagya,walipinga kupunguziwa adhabu mtuhumiwa huyo.
Wakili Kariongi alisema kesi inayomkabili mtuhumiwa huyo ni ya uhujumu uchumi na ambacho amekuwa akifanya muda mrefu ni kuuwa Twiga ambao ni kivutio cha Utalii nchini lakini pia mnyama huyo anachangia pato la taifa.
Alisema wanyamapori huchangia kupatikana fedha za kigeni ambazo ndizo zinachangia kupatikana fedha za miradi ya serikali ikiwepo ujenzi wa shule, kuchangia gharama za afya na nyingine.
Katika kesi hiyo, Jamuhuri ilikuwa na mashahidi saba ambao walikuwa ni mtunza vielelezo vya polisi, Askari wawili walioshiriki kumkamata , Mtambuzi na mtathimini wa nyara za serikali, Mtaalamu kutoka Forensic, Mpelelezi wa kesina Mlinzi wa Amani ambaye alikuwa ni hakimu.
*Wapongeza hukumu* .
Baadhi ya wadau wa sekta ya Utalii na Uhifadhi, wilayani Babati, wakizungumza na waandishi wa habari baada ya hukumu hiyo, walipongeza mahakama kwa uamuzi huo.
Lazaro Peter ambaye ni mhifadhi, alisema biashara ya nyama za Twiga ilikuwa imeshamiri wilayani Babati, kutokana na uwindaji haramu na sasa wanaimani itakuwa imekomeshwa.
“Unajua Twiga wapo wengi sana eneo la Burunge WMA sasa majangili imekuwa ni rahisi kuwawinda na kufanya biashara ya Nyama sasa Meja alikuwa mmoja wa watuhumiwa wakubwa na anatuhumiwa kuuwa zaidi ya Twiga watano kila mwezi”alisema
Meneja wa taasisi ya Chem chem association, ambaye imewekeza katika eneo hilo, Clever Zulu alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kutiwa hatiani ni jitihada ambazo zimefanywa na askari wa Wanyamapori.
Zulu amesema kabla kufanikiwa kukamatwa majangili katika eneo hilo, askari hao wa Wanyamapori walipata mafunzo maalum kutoka kwa maafisa wa TAWA na jeshi la polisi jinsi ya kufanya upelelezi, upekuzi na ukamataji wa majangili.
"Haya ni mafanikio makubwa kwetu katika kulinda rasilimali tunawapongeza askari kwa kuonesha ufanisi baada ya mafunzo"amesema
Zulu amesema Chem chem association ambayo inatumia zaidi ya sh 400 milioni kila mwaka katika kupambana na ujangili katika eneo la Burunge WMA itaendelea kutoa fedha za kupambana na ujangili.
Hadi sasa zaidi ya watuhumiwa 10 wa ujangili wamekamatwa katika eneo hilo na tayari watatu wamehukumiwa vifungo mbali mbali ikiwepo Meja aliyefungwa miaka 23.
No comments:
Post a Comment