ANZIA SOKONI MALIZIA SHAMBANI INAVYOWANUFAISHA WAKULIMA WILAYANI MOSHI MKOANI KILIMANJARO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 20 November 2023

ANZIA SOKONI MALIZIA SHAMBANI INAVYOWANUFAISHA WAKULIMA WILAYANI MOSHI MKOANI KILIMANJARO




Kikundi Cha wakulima wa kijiji Cha Masaera katika picha ya pamoja na viongozi wa JICA pamoja na Ubalozi wa Japan walipotembelea kikundi hicho kuona namna mradi wa Tanshep ulivyoweza kuwanufaisha


Selina Minja mkulima mnufaika wa Mradi wa Tanshep akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea  kikundi hicho hivi karibuni



NA: Andrea Ngobole, Moshi

maipacarusha20@gmail.com



Wakulima wa kijiji cha Masaera wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro wamenufaika na elimu ya kilimo biashara inayotolewa na shirika la kimataifa la maendeleo la Japan (JICA) kupitia mradi wa Tanshep.



Katika mradi huo wa kuimarisha Mipango ya maendeleo ya kilimo unaosimamiwa na halmashauri ya wilaya ya Moshi kwa vikundi vya wakulima umewawezesha wakulima hao kutambua umuhimu wa kilimo biashara kwa kuanzia sokoni na kumalizia shambani kwa kipato Zaidi.



Mkulima wa kijiji hicho, Selina Minja amesema hapo awali walikuwa wanalima kwa mazoea ila toka Mradi wa TANSHEP uwafikie umekuwa na manufaa makubwa kwa sababu wanachokilima kinakuwa kimeshanunuliwa hivyo kuepukana na hasara za mazao yao kutokupata soko.



Aidha ameishukuru Jica kwa kuwanufaisha kwa ujio wa mradi huo na kuwaomba kuwafikia wakulima wengine nchini.



Mkulima mwingine Prosper Tira anasema kilimo cha Tanshep kimemsaidia namna bora ya kutafuta masoko kabla ya kuanza kulima na wamejengewa uwezo wa kufahamu kalenda ya uzalishaji wa mazao kwa majira husika katika kipindi Cha mwaka pia kumfahamu mnunuzi wa mazao kabla ya kuanza kulima.



Anasema wao kama kikundi wamepata elimu ya kilimo biashara kwa kulima mazao ndani ya Greenhouse ambapo walianza na zao la nyanya, ambapo waliuza na kujipatia faida kubwa kama kikundi.



Afisa kilimo na mratibu wa mradi wa kuimarisha mipango ya maendeleo ya kilimo ya wilaya na uwezekaji kwa kutumia mbinu ya SHEP (TANSHEP) wa halmashauri ya wilaya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Hamza Mwinyihija anasema kuwa kilimo biashara kimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wengi kufahamu Hali ya soko na namna ya kulima kulingana na uhitaji wa zao husika.



Amesema wao kama halmashauri wameweza kunufaika kupitia mradi huo kwa wakulima wengi zaidi kujifunza mbinu mpya za kilimo kutoka mbinu ya kizamani ya kuzalisha na kuanza kuuza na kwenda kwenye kuzalisha ili uuze.


Amesema mradi wa TANSHEP umesaidia kuongeza vikundi vya wakulima katika halmashauri ya Moshi wanaonufaika na elimu ya kuanzia sokoni malizia shambani ambapo wamekuwa wakiwasisitiza wakulima kuacha kilimo cha mazoea na kufanya kilimo biashara.


Kauli mbiu ya anzia sokoni malizia shambani inaimarisha ulimaji wa mazao kulingana na mahitaji ya soko ili kubadilisha kilimo kutoka kulima na kuuza kwenda kulima kwa ajili ya kuuza.

Mwakilishi Mkuu wa shirika la maendeleo la kimataifa la Japan (JICA), Ara Hitoshi amesema kuwa mradi wa Tanshep umewanufaisha wakulima 3,000 wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga na kuongeza vipato kwa vikundi vya wakulima kwa asilimia 25.   

“Wakulima lazima wafanye utafiti wa soko kwanza kabla ya kuanza kilimo chochote ili kuwa na uhakika wa soko, kwa kufanyia utafiti wa soko kabla ya kuanza uzalishaji wa mazao yanayohitajika sokoni.” Alisema Ara Hitoshi








No comments: