WANANCHI WAHIMIZWA KUTEMBELEA MAONYESHO YA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA YANAYOENDELEA MKOANI ARUSHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 22 November 2023

WANANCHI WAHIMIZWA KUTEMBELEA MAONYESHO YA WIKI YA HUDUMA ZA KIFEDHA YANAYOENDELEA MKOANI ARUSHA







Na Elinipa Lupembe, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, ametembelea Mabanda ya Maonesho ya tatu ya Wiki ya Huduma za Kifedha, yanayoendelea kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abed Jijini, Arusha, na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi, kutembelea maonesho hayo muhimu ili kupata ufahamu wa huduma sahihi za kifedha.

Mhe. Mongella amesema kuwa maonesho hayo ni muhimu kwa Umma na kuwataka wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani, kufika kwenye mabanda hayo ili kupata elimu ya huduma sahihi na rasmi za kifedha pamoja na kuzitambua taasisi zinazotoa huduma za kifedha ili kuepukana na taasisi za kitapeli.

Ameweka wazi, kuwa kumekuwa na changamoto ya uelewa mdogo wa wananchi, juu ya huduma za kifedha na kusababisha baadhi yao kutapeliwa, kwa kujiingiza kwenye mikopo inayoumiza, na baadaye kuingia kwenye migogoro ya kisheria bila kutegemea, na kusisitiza kuwa maonesho hayo ndio sehemu sahihi ya kupata uelewa na kufanya maamuzi ya kuchagua huduma sahihi na inayofaa.

"Niwasihi wananchi wote, kufika kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid, licha ya kupata elimu juu ya huduma za kifedha, zaidi ni fursa ya kuzitambua taasisi rasmi za kifedha ili kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuchagua huduma ipi ya kuitumia" Amebainisha Mhe. Mongella.

Naye Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Janeth Hiza, amefafanua kuwa, maonesho hayo yana lengo la kutoa elimu kwa Umma, juu ya Huduma za kifedha pamoja na kuwajengea uwezo wa kuelewa juu ya matumizi sahihi ya huduma rasmi za kifedha, zitakazosaidia katika utunzaji wa fedha zao, matumizi ye fedha, kuweka na kukopa, ili kukuza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake.

Inafahamika kuwa, Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 - 2029/30, ambao Elimu kwa Umma ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wake.

Aidha, Maonesho ya Tatu ya Wiki ya Huduma za Kifedha Mwaka 2023 yenye Kauli Mbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Uchumi, yameratibiwa na Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wa wadau wengine wa fedha wakiwemo benki kuu ya Tanzania huku jumla ya Benki 35 zikishiriki na kutoa fursa kwa wananchi kuzifahamu benki hizo na huduma zake.






































No comments: