BARABARA YA LAMI KUINGIA LANGO LA MACHIMBONI MIRERANI KUJENGWA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 21 November 2023

BARABARA YA LAMI KUINGIA LANGO LA MACHIMBONI MIRERANI KUJENGWA

 



Na Mwandishi wetu, Mirerani


maipacarusha20@gmail.com


BARABARA ya kutoka mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara hadi lango kuu la ukuta unaoingia na kutoka kwenye migodi ya madini ya Tanzanite kuanza kujengwa.


Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita moja itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, hivi sasa kwa kugharimu kiasi cha fedha cha shilingi bilioni moja.


Meneja wa TARURA Wilayani Simanjiro, mhandisi Naftal Chaula akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Madini Anthony Peter Mavunde amesema barabara hiyo imeshapata mkandarasi wa ujenzi.


Mhandisi Chaula amesema hatua waliyofikia ni mkataba kusainiwa wanafanya kazi ya kusanifu ili ujenzi wa barabara hiyo uanze mara moja kwa mwaka huu wa fedha.


Amesema wameshachukua udongo na kuupeleka maabara ya TANROAD mkoani Kilimanjiro na ukishapimwa na kutolewa majibu wataanza kufanya kazi ya ujenzi wa barabara hiyo.


“Pia tumezungumza na wenzetu wa TANROAD mkoani Manyara, ili tushirikiane nao, kwani hali ya maji ni mbaya kwa hapa hivyo waongeze karavati lingine kudhhibiti hali hiyo,” amesema mhandisi Chaula.


Amesema mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ya lami unaonyesha kuwa ulipaswa kuanza mwezi Septemba mwaka 2023 na kumalizika Februari mwaka 2024.


Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Cathbert Sendiga amesema fedha za ujenzi wa barabara hiyo shilingi bilioni moja ni kati ya shilingi bilioni 6 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara za wilaya hiyo.


Sendiga amesema fedha hizo ni matengenezo ya barabara za changarawe, makalavati na madaraja hivyo ni matarajio ya Serikali changamoto ya miundombinu hiyo itatatuliwa.



No comments: