CMSA YATOA TAHADHARI YA UPATU HARAMU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 21 November 2023

CMSA YATOA TAHADHARI YA UPATU HARAMU

 



Na Mwandishi wetu, Arusha 


maipacarusha20@gmail.com


MAMLAKA ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) imeitaka jamii kujihadhari na upatu haramu kwani ni hatari kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.


Meneja uhusiano wa CMSA Charles Shirima ameyasema hayo jijini Arusha akizungumza kwenye maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa.


Shirima amesema jamii ijihadhari na matapeli wanaoahidi watu kuvuna pesa nyingi kirahisi hivyo waepuke kupoteza pesa ya jasho lao kupitia upatu haramu.


"Kutokana na hali hiyo watanzania wanapaswa kujiinga kwenye masoko ya mitaji kwani ni sehemu ya mfumo wa sekta ya fedha unaowezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo ya muda mrefu yaani mwaka mmoja," amesema 


Amesema fedha za maendeleo hupatikani kwa kuuza hisa za kampuni, hatifungani za kampuni na vipande katika uwekezaji wa pamoja.


Mchambuzi fedha mwandamizi wa CMSA, Witness Gowelle amesema kupitia maadhimisho hayo wametoa elimu kwa wajasiriamali mbalimbali ili kuwajengea uwezo zaidi.


"Elimu mbalimbali tuliyotoa kwa wajasiriamali watanufaika nao kupitia masoko ya mitaji ili kujiepusha na upatu haramu," amesema Gowelle.


Mjasiriamali wa kutoka wilayani Ngorongoro, Sas  Kotete amesema wajasiriamali wengi wameathirika kupitia upatu haramu hivyo elimu waliyoipata kutoka CMSA itawasaidia kuepuka hayo.


Mjasiriamali mwingine wa mkoani Arusha, Naini Losusu ameipongeza CMSA kwa kuwapa elimu hiyo kwani inawajengea uwezo zaidi juu ya upatu haramu 


Maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa kupitia kauli mbiu ya elimu ya fedha, msingi wa maendeleo ya uchumi, yanafanyika jijini Arusha, kwa siku sita kuanzia Novemba 20 hadi 26 mwaka huu.


Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kufungua rasmi maadhimisho hayo Novemba 22 jijini Arusha 


No comments: