Hatma ya Uhalali pori la Akiba la Pololeti kujulikana Novemba 22 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 14 November 2023

Hatma ya Uhalali pori la Akiba la Pololeti kujulikana Novemba 22

Wakili wa wananchi hao Alute Mughwai akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama kuu Arusha



 


Na: Andrea Ngobole, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Mahakama kuu Kanda ya Arusha itatoa maamuzi kufuatia ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali kudaiwa kutoa tamko ambalo linapotosha maamuzi ya Mahakama kuhusu pori la akiba pololeti November 22 Mwaka huu.


Maamuzi hayo yanafuatia waleta maombi wanane wa Ngorongoro wanaowakilishwa na Mawakili Joseph Ole Shangay, Yonas Masiaya na Denis Moses.


Wananchi hao wameeleza Mahakamani hapo kuwa tamko la mwanasheria Mkuu wa Serikali la Octoba 4, mwaka huu juu ya maamuzi ya Mahakama kuhusiana na uhalali wa pori la akiba la Pololeti limepotoshwa.


Wakili Masiaya alisema tamko hilo limetolewa kinyume cha maadili kwa sababu linapingana na maamuzi ya Mahakama ambayo ilitaka kusimama shughuli zote ndani ya pori la akiba la Pololeti  Hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kama Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali haikubaliani na maamuzi hayo ilipaswa kukata rufaa.


"Mahakama ina wajibu wa kulinda maamuzi yake ili Umma uendelee kuwa na Imani na mahakama, hivyo tunataka amri ya Mahakama kusimamisha shughuli za pori la akiba kutekelezwa "alisema


Hata hivyo, Jaji Mwaseba baada ya kupokea hoja za Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa serikali alipanga November 22 kutoa maamuzi ya shauri hilo.


Wakati huohuo Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imepanga Novemba 24 mwaka huu, kusikiliza na kutoa maamuzi madogo juu ya kesi ya wakazi wanane wa Ngorongoro kuomba kuachiwa Mifugo zaidi ya 1000 ambayo inashikiliwa katika pori la Akiba ya Pololeti wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.


Katika maombi ya shauri hilo namba 106 la mwaka 2023 wanaoshitakiwa na kutakiwa kurejesha mifugo hiyo ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala na maafisa wa Serikali Pius Rwiza, David  Mkenga, Robert Laizer na Prisca Ulomi.

Wakazi wa Ngorongoro wakiwa mahakamani wakimsikiliza shauri lao mapema leo

Wananchi hao wa Ngorongoro waliofungua shauri hilo ni ,Latang  Amwakindwati, Kileo Mbilika, Namuru Kitupei, Philemon Ngulumai, Nokorenta Onyia, Metiantikw Sepena na Saitoti Parmwat.


Wakili wa wananchi hao Alute Mughwai, mbele ya Jaji Nyigulila Mwaseba alisema wateja wake  wamewasilisha maombi ya dharura kuomba kurejeshewa Mifugo hiyo ambayo imekamatwa kinyume cha sheria.


Alisema washitakiwa hao wamekiuka amri ya Mahakama kwa kukamata mifugo hiyo licha ya Mahakama kusitisha ukamataji wa Mifugo na watu katika eneo la Pori la Akiba Pololeti mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.


Hata hivyo , Wakili wa washitakiwa hao watano, Kapimpiti Mugalula  aliomba mahakama kuu kabla ya kutoa maamuzi apate muda wa kupitia hoja za waliopeleka shauri hilo Mahakamani.


"Mheshimiwa Jaji kwa kuwa Leo ndio nimeanza kuwatetea washitakiwa naomba nipate fursa ya kupitia maombi haya ili niweze kuwasilisha hoja kinzani ndani ya siku Saba" amesema


Wakili Mugalula alisema kwa kuwa Mifugo imeshikiliwa hifadhini kuna taratibu za kuachiwa ambazo  hazipo katika Mamlaka ya wanaolalamikiwa.



Hata hivyo, Wakili Mughwai alisema wanaoshitakiwa ndio wanajua wameiweka wapi Mifugo hiyo  na waaomba Mahakama kwa kuzingatia kifungu namba 68 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai kutoa maamuzi ya dharura wakati bado kesi ya msingi inaendelea.


Hata hivyo,Jaji Mwaseba alisema ili aweze kutoa maamuzi ambayo yatatekelezeka ni muhimu upande wa walalamikiwa kupata fursa ya kutoa majibu kinzani.


"Hivyo Novemba 24 saa Tano asubuhi tutapokea hoja kinzani katika shauri hili kabla ya kutoa uamuzi"alisema



Baadhi ya wakazi wa Ngorongoro wakiwa katika Mahakama kuu Arusha mara baada ya kusikilizwa kwa mashauri yao yatakauotolewa maamuzi November 22 na 24 na Jaji Mwaseba

Wakili Munghwai akizungumza na mtetezi wa wafugaji na Mkurugenzi wa shirika la Cilao, Odero Charles nje ya Mahakama hiyo


No comments: