Jowuta na UTPC wataka waandishi habari kulindwa - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 2 November 2023

Jowuta na UTPC wataka waandishi habari kulindwa

Rais wa umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini UTPC Deo Nsokolo 


Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma 




Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com


Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA)  na Muungano wa klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC) wamewataka waandishi nchini kulindwa dhidi ya Uhalifu.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Leo, Rais wa UTPC Deo Nsokolo na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma  wameeleza wakati  duniani inaadhimisha siku ya kupinga uhalifu dhidi ya waandishi wa habari ni muhimu wanahabari walindwe na matukio ya uhalifu.

Kwa majibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Leo na kusainiwa na  mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma, Imesema kuwa Waandishi wa habari Duniani bado wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama na hivyo kujikuta wakifanyiwa uhalifu.



Taarifa hiyo inabainisha kuwa waandishi wa habari wanaendelea kuuawa katika matukio mbalimbali ikiwepo vita, na kushuhudia waandishi wakikamatwa na kufungwa wakiwa wanatimiza majukumu yao.


JOWUTA imebainisha athari ya vita vinavyoendelea nchini Palestina na Israel hadi sasa waandishi 34 wameuawa kwa mujibu wa shirikisho la waandishi duniani.


Juma amesema pia taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)  inasema kuna ongezeko la mauaji ya waandishi wa habari duniani.

Amesema mathalani UNESCO inaeleza mwaka 2018 idadi ya vifo ilikuwa 99 na kisha kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 idadi ikapungua hadi vifo 58 kila mwaka, kwa mujibu wa Kitengo cha UNESCO cha kufuatia mauaji ya waandishi wa habari. 


Taarifa hiyo imeeleza kuwa UNESCO inasema idadi hiyo ya vifo ni kumbusho juu ya pengo katika mifumo ya kisheria duniani kote na kushindwa kwa serikali kutekeleza wajibu wake wa kulinda wanahabari na kuwakinga dhidi ya uhalifu na wakati huo huo kufungulia mashtaka wale wanaotenda uhalifu dhidi ya watumishi hao. 


JOWUTA imeeleza hata hivyo hali ya ukatili dhidi ya waandishi ipo nchi nyingi duniani ikiwepo Tanzania ila ikitofautiana kwa viwango.


Wameeleza kwa mujibu wa utafiti  uliofanywa na baraza la habari Tanzania (MCT) kuhusu madhila ya waandishi katika kipindi cha miaka kumi (2012 – 2022) umebaini ni kunyimwa taarifa waandishi, kutishiwa, kukamatwa, chombo cha habari kufungiwa, kutekwa, kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri.

 

JOWUTA imefafanua kuwa matukio mengine ya madhila dhidi ya waandishi ni kupigwa faini kwa chombo cha habari, vifo, kuharibiwa vifaa vya kazi, kuondolewa katika eneo la tukio kinyume cha sheria na kujidhibiti (self-censorship).


Amesema taarifa ya MCT inasema katika kipindi cha miaka hiyo kumi  jumla ya waandishi wa habari 272,walifanyiwa madhila ya aina mbalimbali kati yao wanaume 219 na wanawake 53 .


Lakini pia tafiti nyingine zinaonesha zaidi ya asilimia 80 ya waandishi  nchini Tanzania hawana ajira wala mikataba hali ambayo inachochea kufanyiwa madhila wanahabari.


Juma anasema JOWUTA , inaungana na wanahabari Duniani kupinga uhalifu dhidi ya waandishi wa habari Ikiwepo kutopewa mikataba ya ajira, kutolipwa mishahara na kukamatwa ama kutishwa kinyume cha sheria.


Amesisistiza kuwepo kwa sheria rafiki dhidi ya wanahabari zikiwepo za kitaaluma na maslahi lakini pia kuwepo sheria ya kuwatambua na kuwalinda watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo wanahabari.


Naye Rais wa umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini UTPC Deo Nsokolo amesema kuwa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC), kutumia klabu za Waandishi wa Habari nchini kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari katika jamii ili kusaidia kupunguza hali ya uhasama dhidi ya waandishi wa habari.


 

"Naomba kusisitiza umuhimu wa kuelimisha umma juu ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya waandishi wa habari katika jamii. UTPC na klabu zake zote na kwa kushirikiana na wadau wengine tunapaswa kuhakikisha kwamba umma unaelewa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari,"Amesema.


Amesema kwa kufanya hivyo ufahamu wao juu ya jinsi vyombo vya habari vinavyochangia kujenga jamii yenye habari na taarifa sahihi na uelewa sahihi utaongezeka na kusaidia kuzuia misimamo ya upande mmoja na kupotosha habari.


Nsokolo amesema umma ulioelimishwa unaweza kushiriki zaidi katika mchakato wa kisiasa na kijamii na hivyo kuwa na mchango mzuri sana katika ujenzi wa taifa. "Kwa kuelewa jukumu la waandishi wa habari katika kuchunguza masuala ya umma, umma unaweza kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao".


Amesema vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kufichua uhalifu na ufisadi hivyo kuelimisha umma juu ya jinsi waandishi wa habari wanavyochunguza na kuripoti masuala hayo kunaweza kusaidia katika kupambana na vitendo hivyo visivyo vya maadili.


"Umma unaoheshimu na kuelewa umuhimu wa vyombo vya habari huru unaweza kuchangia katika kudumisha demokrasia thabiti kwa kushiriki kwa ufahamu katika mchakato wa uchaguzi na kutoa maoni kuhusu sera na masuala ya umma, ambayo ni muhimu katika ujenzi wa taifa". Amesema.


Pia amesema vyombo vya habari vina jukumu la kuchunguza na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadam ambapo kusaidia kugundua na kusimamia haki za binadamu kunaweza kusaidia katika kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. 


Nsokolo pia amezishukuru taasisi mbalimbali ikiwemo Ubalozi wa Uswiss hapa Tanzania, kwa ufadhili wa miradi mbalimbali, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camillus Wambura, kwa kuendelea kushirikiana na UTPC katika kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari hapa nchini unakuwepo na hivyo kuwawezesha kuendelea kutimiza jukumu lao la kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


"Kuanzia mwaka jana, UTPC na Jeshi la Polisi tunaendelea kufanya midahalo na Jeshi la Polisi na kukubaliana mikakati ya ulinzi na usalama wa waandishi. Waratibu wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC), kwa kuendelea kuratibu na kuyatolea taarifa matukio matukio ya ukiukwaji wa uhuru wa kupata na kutoa taarifa na madhila yanayo wapata waandishi wa habari hapa nchini," Amesema.


Nsokolo amemalizia hotuba yake kwa kutoa wito kwa vyombo vya dola vyenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, vichunguze matukio ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.  

No comments: