Na Elinipa Lupembe - Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Albano Mussa, amewataka walimu wa shule za Msingi mkoani humo, kuwasimamia wanafunzi katika masomo ili kupandisha kiwango cha ufaulu, pamoja na utunzaji wa vifaa vya shule, ikiwemo miundombinu.
Mussa ameyasema hayo wakati akizungumza na walimu wa shule Msingi Kalolen, Kata ya Majengo, Halmashauri ya Meru, Mkoa wa Arusha, mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, mradi uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 106.2, kupitia program ya BOOST.
Amesema kuwa walimu wanalo jukumu kubwa la kuwasimamia wanafunzi katika masomo ili waweze kufaulu vizuri, kusimamia nidhamu pamoja na utunzaji wa vifaa vyote vya shule, ikiwemo miundombinu, kwa kuwa, serikali inafanya kazi kubwa ya kuwezesha uwepo wa mazingira bora ya ufundishaji kwa walimu na ujifunzaji kwa wanafunzi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu bora kwenye shule nchini.
“Serikali imefanya sehemu yake ya kuwekeza miundombinu bora na rafiki shuleni, kazi iliyobaki tunawategemea ninyi walimu, kuwasimamia watoto wetu, kuwa na nidhamu, uadilifu na kujituma ili waweze kufaulu vizuri, kwa manufaa ya Taifa letu” amesisitiza.
Aidha, amewahimiza walimu na jamii nzima, kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwa kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu ikiwemo kuwasimamia wanafunzi kuzingatia suala la usafi kwa kutokuchora kuta za ndani na nje za vyumba vya madarasa hayo ili kuendelea kuwa muonekano mzuri kwa muda mrefu.
Hata hivyo walimu hao licha ya kuishukuru Serikali kwa kuwajengea vyumba hivyo vya madarasa, wameiomba serikali kuwajengea nyumba za walimu ili kuwawezesha kutekeleza majuku yao kwa urahisi kwani shule ipo mbali na maeneo ya makazi yao hali inayossababisha kuchelewa kuingia kwenye vipindi na kuzorotesha ufaulu wa wanafunzi.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutujengea madarasa ambayo yatawapa fursa wanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa hapo awali, wanafunzi walilazimika kupokezana kuingia darasani kutokana na uhaba wa madarasa, lakini sasa tunaamini ufaulu utaongezeka” Amesema mwl. Ratibu Shekaratha.
Aidha, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Neema Hekarat ameahidi kusimamia suala usafi kwenye miundominu hiyo pamoja kusimamia kupandisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi hasa kupitia miihani mbali mbali ya kujipima na kuvuka kwenye asilimia 31.2 ambazo shule hiyo imepata, kwenye matokeo ya upimaji wa mtihani Taifa wa kujipima wa darasa la saba mwaka 2023.
No comments:
Post a Comment