Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
AFISA madini mkazi wa Mirerani (RMO) Nchagwa Chacha Marwa, amezikutanisha pande mbili, zenye mgogoro wa kugombea eneo la mgodi wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara.
RMO Chacha amewakutanisha ofisini kwake watu hao wawili Patrick Miroshi (Kipaa) na Joseph Lema wa kampuni ya Njake Enterprises ambayo kwa hivi sasa ndiyo inamiliki mgodi huo.
Mgodi huo wa madini ya Tanzanite unaolalamikiwa na Patrick Miroshi (Kipaa) upo kwenye leseni namba PML 00416SMN ya Lema inayomilikiwa na kampuni ya Njake Enterprises.
Akieleza baada ya kukutana na pande hizo mbili RMO Chacha amesema mazungumzo yao yameanza vyema kwani wote wameitikia wito huo na kukubali kukaa naye kwa pamoja.
“Tumeanza vyema mazungumzo yetu na kila mmoja kati ya watu hao wawili, ameeleza bayana juu ya namna anavyofahamu juu ya mgodi huo unaolalamikiwa,” amesema RMO Chacha.
Hata hivyo, amesema suala hilo limeshafikishwa kwenye vyombo vya kisheria, hivyo wameongelea masuala ambayo hawawezi kuingilia uhuru wa mahakama.
Hivi karibuni mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Patrick Miroshi (Kipaa) alilalamika kwa Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde kunyang’anywa mgodi wake aliouchimba kwa zaidi ya miaka 20.
Waziri Mavunde baada ya kusikiliza lalamikio hilo, akamuagiza RMO Chacha, kuingilia kati mgogoro huo, kuusikiliza na kuutatua kwa kuzikutanisha pande mbili hizo.
No comments:
Post a Comment