REGROW KUENDELEZA UHIFADHI WA MISITU NA KUINUA UCHUMI KUPITIA UFUGAJI NYUKI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 10 November 2023

REGROW KUENDELEZA UHIFADHI WA MISITU NA KUINUA UCHUMI KUPITIA UFUGAJI NYUKI

 






Na Anangisye Mwateba,Dodoma


maipacarusha20@gmail.com


Mradi wa kuendeleza utalii kusini (REGROW) utaendelea kuimarisha uhifadhi wa misitu na kuinua uchumi kwa wananchi wa nyanda za juu kusini  kupitia ufugaji nyuki.


Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (MB) wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Jesca Jonathani Msambatavangu ambaye alitaka kujua  je Serikali haioni umuhimu wa kugawa mizinga ya nyuki ili kubadili shughuli za kiuchumi zinazoharibu mazingira kama kukata miti na mkaa Iringa?


Mhe Kitandula alifafanua kuwa Serikali kupitia Mradi wa REGROW imetoa elimu ya Ufugaji nyuki kwa jamii ya Tungamalenga na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kugawa mizinga 50 kwa kikundi cha SUBIRA kilichopo Wilaya ya Iringa.


Vilevile Mhe. Kitandula amesema kuwa Elimu ya ufugaji Nyuki imeendelea kutolewa kwa jamii zinazozunguka hifadhi ambapo kupitia elimu hiyo wananchi wamefundishwa namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji nyuki kwa tija. 


“Mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ilitoa mizinga 269 yenye thamani ya shilingi milioni 26.9 kwa vikundi 19 vya wafugaji nyuki katika Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi” Aliongeza Mhe. Kitandula


Aidha Mhe. Kitandula amesema kwamba  Mfuko wa Misitu Tanzania umetoa ruzuku ya Shilingi Million 20 kwa vikundi 2 vya ufugaji Nyuki vilivyopo Wilaya ya Iringa lakini pia umekuwa ukitoa tangazo na kupokea maombi ya ruzuku zitolewazo kwa wadau wa misitu na ufugaji nyuki na sasa unaendelea kupokea maombi ya ruzuku.


Awali Mhe Kitandula akijibu swali la Mbunge wa Donge Mhe. Soud Mohammed Jumah ambaye alitaka kujua Je, kuna mkakati gani wa kupunguza athari hasi zitakazojitokeza kutokana na kuondoshwa kwa buffer zone katika hifadhi na mapori.


Mhe Kitandula alifafanua kuwa katika kupunguza athari za kutokuwa na maeneo ya kinga, Wizara kupitia taasisi zake za uhifadhi (TANAPA, TAWA, na NCAA) inatoa elimu kwa wananchi kuhusu kutokuanzisha shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na makazi kwenye maeneo ya karibu na hifadhi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori.


Pia amesema  pamoja na kuwaelimisha wananchi lakini serikali imekuwa ikiwataka  kuanzisha shughuli rafiki kama vile ufugaji nyuki, kupanda miti kwa ajili ya hewa ukaa na kuendesha utalii wa kiutamaduni.


Amefafanua kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kushirikiana na serikali za vijiji na halmashauri kuweka mipango bora ya matumizi bora ya Ardhi  na kuendelea kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ili kulinda wananchi na mali zao.

No comments: