Wakulima waiomba serikali kupiga jeki elimu ya kilimo Ikolojia - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 22 November 2023

Wakulima waiomba serikali kupiga jeki elimu ya kilimo Ikolojia

 


Na Mwandishi Wetu, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Baadhi wa wakulima kutoka wilaya za Arumeru na Karatu mkoani Arusha wameiomba serikali kuwawezesha kwa kuwapa elimu ya mafunzo ya kilimo Ikolojia kinacholenga kuangalia ustawi wa kilimo na mlaji.

Wakiongea na waandishi wa habari katika zihara maalumu ya kutembelea vikundi ambavyo viko chini ya mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji Mkoa wa Arusha (Mviwaarusha),wakulima hao wameonyesha nia ya kuhitaji kupatiwa zaidi elimu ya kilimo ikolojia ambayo inalinda na kuheshimu mahusiano ya viumbe hai na mazingira ili kumwezesha matokeo chanya ya kiafya,kiuchumi,kijamii na kimazingira.

Loma Lotasaruaki ni mwenyekiti wa mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji wa kijiji cha Ekenywa (Mviwaeke),kilichopo wilayani Arumeru alisema kilimo hicho cha kutumia mbegu,mbolea na dawa za asili ni rafiki kwa mkulima kwani kinawaepusha na magonjwa mbali mbali yatokanayo na mazao ambayo yanatengenezwa na kupuliziwa kemikali.

Alisema tangu walipoanza kilimo hicho wamepata faida mbali mbali ikiwemo kujiokoa kwenye matumizi ya vyakula vyenye kemikali ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu lakini pia kwao imekuwa ni fursa ya kujiingizia mapato.

Aliongeza kupitia mtandao wao ndani ya miaka mitatu wamekuwa na uwezo wa kuuza miche ya miti 25000 hadi 35000 kwa mwaka lakini pia wameweza kupata mashine ya kuchataka mafuta ya alizeti huku akikiri changamoto kubwa ni wakulima wengi bado hawana elimu ya kutosha.

“Hapa tuna miti mingi ambayo ni rafiki kwa utunzaji wa mazingira lakini pia zile ambazo zina rutubisha ardhi ambazo ni rafiki lengo ni kurudisha uoto wa asili ndio maana unaona tumekuwa tukitoa elimu japo tunaitaji sapoti kutoka serikalini”,alisema Loma.

Eliza Kivuyo ni mkulima wa kilimo Ikolojia alisema serikali inatakiwa kusaidia katika upande wa kuelimisha wananchi ili kumwezesha kila mtu kutambua zaidi umuhimu wa kilimo icho ambayo pia licha ya kuongeza kipato lakini pia inasaidia katika kupata uoto wa asili.

Alisema bado watu wachache ndio wana elimu juu ya kilimo hicho lakini kama serikali pia itaona umuhimu na kuamua kutoa semina mbali mbali kwa wakulima basi kilimo ikolojia itakuwa ni suluhu ya kuepusha watu na magojwa yatokanayo na mazao yenye kemikali.,

 

Kwa upande wake Florian Gitu mkazi wa Dova Juu wilayani Karatu ambaye ni mkulima na mfugaji anakiri alipojiunga na taasisi ya Mviwaarusha na kupewa mafunzo juu ya faida za kilimo ikolojia kupitia utengenezaji wa miti na kuwezeshwa mtambo wa Biogas maisha yake yamebadilika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

“Biogas imenipatia sana manufaa katika familia yangu kwa sababu inaendana na mifugo kwa maana unatumia kinyesi cha mifugo ambapo kwangu natumia kama nishati ya kupikia nah ii pia inapunguza garama za maish”.

“Kabla sijaipata mke wangu alikuwa anaenda asubuhi kusenya porini ambapo anaweza kukumbana na wanyama wakali lakini sasa mambo yemebadilika anaingia kwenye shughuli za mapishi tu”,aliongeza Gitu.

Naye afisa ugavi kutoka taasisi ya Mviwaarusha,Eliud Letunga alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima na jamii kwa ujumla kuhusu kilimo cha ikolojia ambacho gharama yake ni nafuu kwani kinatumia mbegu na mbolea za asili huku pia wakipambana kuwaelimisha kuhusiana na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ambayo ni uoto wa asili na sasa mwitikio umekuwa wa kuridhisha kiasi chake.

Alisema wamekuwa wakiwaelimisha wakulima hao kuhusu utunzaji wa mazingira,miti ya kusaidia jamii kupata lishe,miti ambayo inarutubisha ardhi lakini pia namna gani watalima kwa kutumia hizo mbegu,mbolea na dawa za asili.

No comments: