WASICHANA SEKONDARI MRINGA WAMSHUKURU MAMA SAMIA KWA KUWAJALI WASICHANA NCHINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 11 November 2023

WASICHANA SEKONDARI MRINGA WAMSHUKURU MAMA SAMIA KWA KUWAJALI WASICHANA NCHINI

 




Na Elinipa Lupembe


maipacarusha20@gmail.com


Wanafunzi wasichana shule ya sekondari Mringa wamemshukuru mama Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa elimu kwa wasichana nchini. 


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shuleni kwao, wamethibitisha kuwa serikali ya awamu ya sita licha ya kuendelea kuboresha mazingira ya elimu nchini lakini imeenda mbali zaidi kwa kujenga miundombinu ya mabweni ya wasichana shuleni, inayowapa fursa watoto wa kike kusoma katika mazingira rafiki na wezeshi.


Simalo Mayenga mwanafunzi wa kidato cha 6, amesema kuwa ujenzi wa mabweni ya wasichana shuleni kwao, unadhihirisha namna Rais mama Samia anavyo wajali na kutoa kipaumbele kwa  wasichana  nchini ili waweze kupata elimu kwenye mazingira mazuri na wezeshi.


"Ujenzi wa mabweni unatuwezesha wasichana kusoma vizuri na kufikia ndoto zetu, ndoto ambazo zilizimwa kwa wasichana wengi kwa kukatishwa masomo kutokana na changamoto mbalimbali za kusoma shule za kutwa, kwa sasa wasichana wamehakikishiwa usalama wao katika safari yao ya masomo " Amesema Asimwe


Britney Baraka, anayesoma ya tahususi ya HGL, amesema kuwa ujenzi wa mabweni mawili shuleni hapo, unatoa fursa kwa wasichana kusoma vizuri na kwa uhuru huku wakiepukana na hatari zinazowapata wasichana wengi wanasoma shule za kutwa.


Naye Asimwe Garasian anayesoma tahususi ya  EGM, amethibitisha kuwa, wanafunzi wa kutwa hukumbana na changamoto nyingi za kijamii njiani, uwepo wa mabweni ya wasichana unatoa fursa kuepukana nazo kutokana na kuishi kwenye mazingira rafiki na kusoma kwa usalama bila kubughudhiwa.


Awali serikali ya awamu ya sita kupitia programu ya kuboresha miundombinu ya shule za sekondari (SEQUIP), imetoa shilingi milioni 360 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mapya mawili na ukarabati wa mabweni manne ya zamani. 


Makamu mkuu wa shule ya sekondari Mringa, Mwl. Kleruu Zakaria Sumaye, amesema kuwa, shilingi milioni 260 zimejenga mabweni mapya mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 160 na 80 kwa kila bweni na milioni 100 zimetumika kukarabati mabweni manne yaliyojengwa zaidi ya miaka 70 iliyopita.

No comments: